Taliban kuigeuza ardhi ya Afghanistan 'makaburi' ya askari wa Marekani
Kundi la wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan limetangaza kuwa litaigeuza nchi hiyo "eneo la makaburi" ya askari wa Marekani baada ya nchi hiyo kutangaza kuwa itaendelea kuikalia kwa mabavu nchi hiyo ya bara la Asia.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake Zabiullah Mujahid, kundi la Taliban limesisitiza kuwa: "Ikiwa Marekani haitaondoa askari wake Afghanistan, karibuni hivi nchi hii itageuka makaburi mengine ya dola hili kubwa katika karne ya 21".
Mujahid aidha ameitaka Washington ifikirie stratijia ya kuondoka "badala ya kuendeleza vita" dhidi ya Afghanistan.
Msemaji wa Taliban amesisitiza kuwa kundi hilo litaendeleza mapambano ya mtutu wa bunduki maadamu atakuwepo askari japo mmoja wa Marekani ndani ya ardhi ya Afghanistan kuendeleza vita dhidi ya kundi hilo.
Onyo hilo la kundi la Taliban limetolewa masaa kadhaa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kubadilisha msimamo wa ahadi aliyotoa hapo awali ya kuhitimisha moja ya vita vilivyochukua muda mrefu zaidi katika historia ya Marekani.
Katika hotuba aliyotoa kwa njia ya televisheni hapo jana mbele ya vikosi vya jeshi la Marekani katika kituo cha jeshi cha Fort Myer katika jimbo la Virginia, Trump alitangaza mkakati mpya kwa ajili ya Afghanistan na kutupilia mbali kile alichokiita "ratiba za kubahatisha" za kuwaondoa askari wa Marekani nchini humo.
Japokuwa hakutoa maelezo zaidi kuhusu idadi halisi ya askari wa ziada wanaoweza kupelekwa huko Afghanistan, Rais wa Marekani aliashiria kuwa anakubaliana na pendekezo la wizara yake ya ulinzi Pentagon la kutuma askari wengine 4,000 huko Afghanistan ambako tayari kuna askari 8,400 wa jeshi la Marekani.
Aidha amesema yuko tayari kufikia makubaliano ya kisiasa na Taliban "wakati fulani" baada ya kufanyika kwanza "jitihada athirifu za kijeshi"…/