Marekani yaendeleza ukatili wake, yaua raia 30 Afghanistan
(last modified Thu, 31 Aug 2017 02:52:28 GMT )
Aug 31, 2017 02:52 UTC
  • Marekani yaendeleza ukatili wake, yaua raia 30 Afghanistan

Makumi ya raia wameuawa katika shambulizi la anga lililofanywa na ndege ya kivita ya Marekani katika mkoa wa Logar, mashariki mwa Afghanistan.

Wakazi wa mji wa Puli Alam, makao makuu ya mkoa huo wamenukuliwa na kanali ya televisheni ya Press TV wakisema kuwa, hujuma hiyo ya jana Jumatano iliua raia kati ya 28 na 32.

Salim Saleh, msemaji wa gavana wa mkoa wa Logar amethibitisha kutokea shambulio hilo la anga la Marekani, ingawaje amesema serikali haina takwimu rasmi za wahanga wa hujuma hiyo kwa sasa.

Wakati huo huo, genge la Taliban limetangaza habari ya kudungua ndege ya Marekani iliyotokeleza hujuma hiyo. Hata hivyo taarifa hiyo haijathibitishwa na serikali ya Afghanistan au jeshi la Marekani.

Ndege za kivita za Marekani

Hivi karibuni, Rais wa Marekani Donald Trump, alitangaza stratejia mpya ya vita ya Washington kuhusiana na Afghanistan sambamba na mpango wa kutuma askari wapya nchini humo.

Trump anatazamiwa kuidhinisha uamuzi wa kutumwa askari elfu nne zaidi nchini Afghanistan. Askari hao wapya wa Marekani watajumuishwa na wenzao 8,400 walioko hivi sasa nchini humo pamoja na wengine elfu tano wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO). 

Tangu Marekani ilipoivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan Oktoba mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi baada ya shambulizi la Septemba 11, harakati za kigaidi zimeonekana kupamba moto katika nchi hiyo siku baada ya siku.