Makumi ya shule zafungwa na magaidi wa Daesh nchini Afghanistan
Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) limefunga shule 73 katika mkoa wa Jozjan, kaskazini mwa Afghanistan sambamba na kupora vifaa vya masomo.
Halima Sadaf Karimi, mjumbe wa Baraza la Mkoa wa Jozjan ametangaza kuwa, shule zilizofungwa na magaidi hao ni za miji ya Darzab na Qush Tepa na kwamba, taarifa iliyotolewa na wanachama wa genge hilo hatari la kigaidi, inasema majengo ya shule hizo yatageuzwa na kuwa ngome zake za kijeshi.
Bi, Halima Karimi ameongeza kuwa hadi sasa wanachama wa Daesh wamepora vitendea kazi vyote vya shule hizo. Abdul Hai Yashin, Mkuu wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Mkoa wa Jozjan amethibitisha habari ya kufungwa shule hizo na kuporwa vifaa vyake kulikofanywa na wanachama wa kundi la Daesh na kwamba vifaa hivyo vimepelekwa katika ngome zao. Hadi sasa zaidi ya shule 1000 katika maeneo tofauti ya Afghanistan zimepigwa kufuli kutokana na machafuko au vitisho vya makundi ya kigaidi.
Afghanistan ina karibu wanafunzi milioni tisa ambapo karibu asilimia 35 ni wasichana wanaosoma katika shule elfu 16 nchi humo. Hata hivyo uwepo wa makundi ya kigaidi ya Taleban na Daesh nchini humo umepelekea aghlabu ya wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo na hivyo kuharibikiwa mustakbali wa maisha yao.