Dec 01, 2017 07:52 UTC
  • UNICEF: Watoto 18 wanaambukizwa HIV/Ukimwi kwa kila saa moja

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema watoto 18 huambukizwa virusi vya HIV katika kila saa moja kote duniani, ishara kwamba jitihada za makusudi zingali zinahitajika kuzuia maambukizi ya virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa hatari wa Ukimwi miongoni mwa vijana na watoto wadogo.

Hayo yamesemwa hii leo na UNICEF, ikitoa ripoti ya maambukizi ya HIV ya mwaka jana, kwa mnasaba wa Siku ya Ukimwi Duniani inayoadhimishwa hii leo. Dakta Chewe Luo, Mkurugenzi wa masuala ya HIV katika UNICEF amesema jinamizi la Ukimwi halijamalizika, na ni jambo lisilokubalika kuona watoto na vijana wanaendelea kupoteza maisha kila siku kutokana na ugonjwa huo.

Amesema takriban watu milioni 37 kote duniani wanaishi na virusi vya HIV, miongoni mwao wakiwa ni vijana milioni 2.1 waliobaleghe; huku vijana 55 elfu wenye umri huo wa kubaleghe wa kati ya miaka 10 na 19, na vile vile watoto wenye chini ya umri wa miaka 14 wapatao laki 1 na 20 elfu wakiaga dunia kutokana na magonjwa ya zina yanayofungamana na Ukimwi mwaka jana.  

Nusu ya watu wanaoishi na Ukimwi duniani hawajapimwa

Kwa mujibu wa UNICEF, virusi vya HIV vingali sababu kuu ya vifo vya vijana barani Afrika, ambapo asilimia 70 ya watu wanaoishi na ugonjwa huo duniani ni vijana kutoka eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.

Hata hivyo Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umepongeza kupungua kwa maambukizi ya virusi hivyo kutoka kwa mama mzazi hadi mtoto, na kwamba maambukizi milioni 2 ya namna hii yamezuiwa tokeo mwaka 2000 hadi mwaka jana 2016.

Nalo Shirika la Afya Duniani WHO limesema karibu nusu ya watu wanaoishi na virusi vya HIV kote duniani hawana habari wala ufahamu kuwa wameambukizwa virusi hivyo hatari vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi.

Tags