Araqchi: Quds ni mji mkuu wa asili wa Ulimwengu wa Kiislamu
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Ni yakini kwamba Quds tukufu ni mji mkuu wa asili wa Ulimwengu wa Kiislamu na utarejea mikononi mwa Umma wa Kiislamu.
Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya kisheria na kimataifa ameyasema hayo leo katika mkutano wa kimataifa uliofanyika hapa mjini Tehran kwa anuani ya "Quds, mji mkuu wa amani wa dini mbalimbali" na kuongeza kwamba Baitul Muqaddas ni kibla cha mwanzo cha Waislamu duniani. Amekumbusha kuwa kadhia ya Quds tukufu, ambayo ni maudhui kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu, inapasa ibaki hai daima.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani pia hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuamuru ubalozi wa Marekani uhamishiwe katika mji huo. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatilia mkazo kila mara msimamo wa kulaani hatua hiyo isiyo na nadhari ya Trump na itaendelea kupinga na kukabiliana na mabadiliko yoyote yatakayofanywa kuhusiana na Quds.
Licha ya upinzani mkubwa kieneo na kimataifa, tarehe 6 Desemba mwaka 2017, Rais wa Marekani alitangaza kuwa: Marekani inaitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa Israel.
Mji wa Baitul Muqaddas ni mahali ulipo msikiti mtukufu wa Al Aqsa ambao ni kibla cha mwanzo cha Waislamu na ni sehemu isiyotenganika na ardhi ya Palestina na ni moja ya maeneo matatu makuu matakatifu ya Kiislamu yenye hadhi na umuhimu maalumu mbele ya Waislamu.
Mji huo ulivamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967.../