Mar 13, 2018 15:52 UTC
  • Russia yaionya vikali Marekani kuhusu kushambulia tena Syria, yasema itajibu

Maafisa wa ngazi za juu wa Russia wameionya vikali Marekani kuwa isithubutu kuishambulia upya Syria kwani matokeo ya chokochoko kama hivyo yatakabiliwa na jibu kali la Russia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov amenukuliwa na Shirika la habari la Itar Tass akiionya Marekani kuhusu matokeo ya hujuma yoyote mpya dhidi ya Syria huku akitahadahrisha kuwa, hatua kama hiyo itakuwa na matokeo mabaya.

Lavrov alikuwa akijibu kauli ya Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley ambaye jana alisema kuna uwezekano wa Marekani kuchukua uamuzi wa upande moja, yaani bila kuishauri jamii ya kimataifa, na kuishambulia Syria.

Aidha Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Russia Valery Gerasimov ameonya kuwa nchi yake itajibu kijeshi hujuma ya jeshi la Marekani dhidi ya Syria. Amesema watalenga zana za kivita zitakazotumiwa kuhatarisha maisha ya wanajeshi wa Russia nchini Syria.

Wanajeshi wa Russia katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Khmeimim nchini Syria

Gerasimov amesema kuna idadi kubwa ya washauri wa kijeshi wa Russia nchini Syria na hivyo Moscow itachukua hatua za kukabiliana na wanaohatarisha maisha yao.

Amesema Marekani inapanga kuituhumu serikali ya Syria kuwa imetumia silaha za kemikali kisha itoe ushahidi bandia na baada ya hapo ipate kisingizio cha kushambulia vituo vya kijeshi nchini Syria. Jenerali huyo wa Russia pia amesema kuna taarifa kuwa magaidi wanapanga kutumia silaha za kemiklia nchini Syria na kisha wailaumu serikali kuwa ndio iliyohusika ili Marekani ipate kisingizio cha kuishambulia upya nchi hiyo ya Kiarabu.

Tags