Putin aamuru mwongozo wa utumiaji silaha za nyuklia wa Russia ufanyiwe mabadiliko
(last modified 2024-09-26T05:09:33+00:00 )
Sep 26, 2024 05:09 UTC
  • Putin aamuru mwongozo wa utumiaji silaha za nyuklia wa Russia ufanyiwe mabadiliko

Rais Vladimir Putin wa Russia ameamuru mwongozo wa utumiaji silaha za nyuklia wa nchi hiyo ufanyiwe mabadiliko akionya pia kuwa nchi yake inaweza kujibu mapigo kwa silaha za nyuklia ikiwa itashambuliwa kwa silaha za kawaida zilizotolewa na dola linalomiliki silaha hizo.

Akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Russia uliorushwa hewani na televisheni ya nchi hiyo, Putin amebainisha kuwa kulingana na marekebisho na mabadiliko yaliyopangwa kufanyika, shambulio dhidi ya nchi hiyo na nchi isiyo na silaha za nyuklia kwa "kushiriki au kuunga mkono dola la nyuklia" litachukuliwa kama "shambulio la pamoja dhidi ya Shirikisho la Russia”.
 
Katika hotuba yake hiyo, Putin hakufafanua ni lini mabadiliko ya Mwongozo wa nyuklia wa Russia yataanza kutumika. Hata hivyo, katika miezi ya karibuni, maafisa waandamizi, akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Sergey Ryabkov na Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov wamekuwa wakijadili mabadiliko yanayoweza kutokea  katika mwongozo huo. Mwishoni mwa Agosti, Waziri wa Mambo ya Nje Sergey Lavrov alisema hati hiyo "inafanyiwa mapitio.
Rais Putin wa Russia akihutubia Baraza la Usalama la nchi hiyo

Mabadiliko hayo yanayoonekana kupunguza kwa kiasi kikubwa kizuizi cha Russia kutumia silaha za atomiki yanakuja wakati washirika wa Magharibi wa Ukraine wakifikiria iwapo wairuhusu Kyiv itumie silaha za masafa marefu kushambulia maeneo ya kijeshi ndani ya Russia, na mwezi mmoja baada ya Kyiv kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza katika eneo la Russia la Mkoa wa Kursk.

 
Russia ndiyo nchi yenye nguvu kubwa zaidi za nyuklia duniani. Kwa pamoja, nchi hiyo na Marekani zinamiliki asilimia 88 ya vichwa vyote vya nyuklia duniani.../

 

Tags