Israel yafanya maangamizi Lebanon, yateketeza msikiti na soko, idadi ya waliouawa na kujeruhiwa haijajulikana
(last modified 2024-10-13T10:57:01+00:00 )
Oct 13, 2024 10:57 UTC
  • Israel yafanya maangamizi Lebanon, yateketeza msikiti na soko, idadi ya waliouawa na kujeruhiwa haijajulikana

Msururu wa mashambulizi ya kinyama ya anga yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel yameteketeza kikamilifu msikiti na kubomoa soko kusini mwa Lebanon, katika kile kilichoelezewa kama "uangamizaji wa kila kitu" huku utawala huo ghasibu ukishadidisha na kupanua mashambulizi yake ya mabomu na makombora katika kila pembe ya nchi hiyo.

Katika shambulizi la karibuni zaidi lililofanywa mapema leo, jeshi la utawala wa Kizayuni limeuteketeza kikamilifu msikiti wa zamani katika kijiji cha Kfar Tibnit kusini mwa Lebanon. Taarifa kamili za idadi ya vifo hazijaweza kupatikana.

Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Lebanon, shambulio jengine lililofanywa usiku wa kuamkia leo kwenye soko lililoko katika mji Nabatieh kusini mwa nchi hiyo limeua shahidi watu kadhaa. Hata hivyo idadi halisi ya waliofariki na kujeruhiwa bado haijajulikana kutokana na moto mkubwa uliosababishwa na shambulio hilo.

Duru za habari zimeripoti kuwa, Shirika la Msalaba Mwekundu la Lebanon lingali linajaribu kuona "kama kuna walionusurika na kujaribu kuwaondoa waliojeruhiwa" kwenye eneo la shambulio.

Mashuhuda wa shambulio hilo la kinyama lililofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wameielezea hali ya maafa kuwa ni sawa na maangamizi kamili kwa sababu mitaa yote ya eneo hilo imeteketezwa.

Ripota wa televisheni ya Al Jazeera Imran Khan ameripoti kutoka Hasbaiyya mkoani Nabatieh akisema: "moto ulikuwa mbaya kiasi kwamba huduma za dharura hazikuweza kuingia na kuona kama kulikuwa na miili kwenye vifusi," na kuongeza kuwa soko la eneo hilo "limeteketea kwa moto kikamilifu".../

 

 

Tags