Kupuuza Mogherini na Putin mchezo wa kitoto wa Benjamin Netanyahu
(last modified Tue, 01 May 2018 12:07:45 GMT )
May 01, 2018 12:07 UTC
  • Kupuuza Mogherini na Putin mchezo wa kitoto wa Benjamin Netanyahu

Ikulu ya Russia Kremlin imetangaza kuwa, Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Benjamin Netanyahuu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Rais Putin amesisitiza katika mazungumzo yake hayo na Netanyahu juu ya ulazima wa kulindwa makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA kwa ajili ya uthabiti wa dunia. Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya mchezo mpya wa kitoto wa Benjamin Netanyahu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya naye amejibu mchezo wa kitoto wa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel aliyedai kuwa eti Iran haijaheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Mogherini amesisitiza kwamba, Iran imeheshimu kikamilifu makubaliano ya nyuklia yanayojulikama kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Jana usiku, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel alionesha picha, CD na karatasi akidai kuwa eti Iran inaendesha kwa siri mpango wa kumiliki silaha za nyuklia. 

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel

Madai hayo ya uongo ya Netanyahu yametolewa mara baada ya ziara ya Waziri wa Mashauuri ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo huko Tel Aviv, kama njia ya kuhalalisha nia ya Rais wa Marekani ya kujitoa kwenye mapatano hayo.  Madai hayo ya Netanyahu ni kukariri madai yale yale ya Marekani kuhusiana na mipango ya nyuklia ya Iran yaliyojulikana kama uwezekano wa kutumiwa kwa malengo ya kijeshi shughuli za nyuklia za Iran (PMD), madai ambayo faili lake lilikwishafungwa na Wakala wa  Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Jambo muhimu katika uwanja huu ni kipindi cha kutolewa madai mapya ya Netanyahu dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani. Inaonekana kuwa, hatua hiyo ni katika fremu ya kushadidisha mashinikio dhidi ya Iran hasa kwa kuzingatia kukaribia muda uliotangazwa na Rais Donald Trump wa Marekani wa kukubaliwa masharti yake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambao ni tarehe 12 ya mwezi huu wa Mei.

Anthony Scaramucci, Mkurugenzi wa zamani wa Mawasiliano wa Donald Trump amedai kwamba: Katika mivutano mikali ya Trump na madola makubwa duniani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia na Iran, Rais huyo atapata mafanikio yale yale aliyoyapata kuhusiana na suala la Korea Kaskazini.

Rais Donald Trump wa Marekani

Kwa kuzingatia mazungumzo ambayo hayajawa na natija ya viongozi wa Ulaya wanachama wa kundi la 5+1 yaani Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pamoja na Rais Donald Trump wa Marekani, hivi sasa Waziri Mkuu wa Israel ametoa madai ya kitoto kwamba, eti Iran inaendesha kwa siri mpango wa kumiliki silaha za nyuklia ili kumshajiisha Trump kadiri iwezekanavyo na hivyo kuimarisha madai dhidi ya Iran.

Vichslav Matazov, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Russia anasema kuwa, lengo la Trump katika kadhia nzima ya makubaliano ya JCPOA ni kumridhisha Benjamin Netanyahuu. Siku zote Israel imekuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa makubaliano ya JCPOA na imekuwa ikipinga kufikiwa makubaliano ya nyuklia na Iran na badala yake imekuwa ikitaka kuongezwa mashinikizo dhidi ya Tehran. Kufikiwa makubaliano ya nyuklia na baadaye makubaliano hayo kupasishwa na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni jambo ambalo lilikabiliwa na radiamali kali ya Israel. Kimsingi ni kuwa, viongozi wa Tel Aviv hawakufurahishwa kabisa na hatua ya kufikiwa makubaliano hayo na ndio maana wamekuwa wakionyesha misimamo mikali inayopinga makubaliano hayo.

wawakilishi wa mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na 5+1

Pamoja na hayo, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yalianza kutekelezwa Januari 2016 na yameendelea kubakia hai hadi leo licha ya njama za kuyakwamisha zinazofanywa na Marekani. Baada ya kuingia madarakani Trump viongozi wa Israel hususan Benjamin Netanyahu walipata matumaini mapya hasa kutokana na misimamo hasi aliyonayo Rais huyo wa Marekani dhidi ya makubaliano hayo ya nyuklia. Kwa mtazamo wa Israel ni kwamba, madai ya Netanyahu kuwa, eti iIran naendesha kwa siri mpango wa kumiliki silaha za nyuklia huenda yakawa na taathira katika propaganda za Trump dhidi ya JCPOA na hivyo kumkinaisha kiongozi huyo wa Marekani kuyavunja makubaliano hayo.

Pamoja na hayo yote, msimamo ulionyeshwa na Rais Vladimir Putin wa Russia na Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya dhidi ya madai ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel ni ithbati kwamba, viongozi hao wanafahamu vyema malengo yaliyoko nyuma ya pazia ya Netanyahu kuhusiana na JCPOA na ndio maana wameyapuuza madai yake hayo.