Kujizuia Ulaya kubeba gharama za kujitoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44378-kujizuia_ulaya_kubeba_gharama_za_kujitoa_marekani_katika_makubaliano_ya_jcpoa
Jean-Yves Le Drian Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ameitaja hatua ya Marekani ya kuyawekea mashinikizo mashirika ya nje ambayo yana uhusiano wa kibiashara na Iran kuwa haikubaliki na kueleza kuwa: Nchi za Ulaya hazipasi kubeba gharama za kujitoa Marekani ndani ya JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 12, 2018 07:55 UTC
  • Kujizuia Ulaya kubeba gharama za kujitoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA

Jean-Yves Le Drian Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ameitaja hatua ya Marekani ya kuyawekea mashinikizo mashirika ya nje ambayo yana uhusiano wa kibiashara na Iran kuwa haikubaliki na kueleza kuwa: Nchi za Ulaya hazipasi kubeba gharama za kujitoa Marekani ndani ya JCPOA.

Le Drian amekosoa hatua hiyo ya Marekani dhidi ya mashirika ya Ulaya yanayoshirikiana na Iran na kubainisha kuwa nchi za Ulaya zinapasa kuunga mkono maslahi ya mashirika yao mkabala na vikwazo hivyo vya White House dhidi ya Iran. 

Msimamo huo mkali wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa kuhusu miamala ya Marekani ya kuzitwisha gharama pande nyingine baada ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia kwa jina la JCPOA khususan washirika wake wa Ulaya unaonyesha kuwa nchi za Ulaya kama ilivyokuwa huko nyuma hazitaki kufuata kikamilifu siasa za Marekani kuhusu Iran na zimedhamiria kwa dhati kuyalinda makubaliano hayo ya kimataifa ambayo yanadhamini malengo yao yaliyokusudiwa. Hata hivyo kulindwa makubaliano ya JCPOA kunakwenda sambamba na kufungamana Iran na makubaliano hayo. Tehran imetangaza kuwa itasalia kwenye makubaliano hayo ya nyuklia iwapo maslahi yake yataendelea kudhaminiwa. Hatupasi kutaraji kuwa Tehran itabakia katika makubaliano ya JCPOA iwapo Marekani itayawekea vikwazo hivyo vya pili mashirika au mabenki na taasisi zisizo za Kimarekani ambazo zitakuwa na mahusiano ya kibiashara, kiuchumi na kibenki na Iran kufuatia kushtadi mashinikizo na vikwazo dhidi ya Iran na serikali kubwa za Ulaya na Umoja wa Ulaya kutochukua hatua katika uwanja huo.   

Iwapo nchi za Ulaya zitakuwa na matarajio hayo hazitapata jibu chanya kutoka kwa Iran. Hivi sasa mpira upo uwanjani mwa nchi za Ulaya ili zikabiliane kwa jadi na Trump ambaye ameamua kujitoa katika makubaliano ya JCPOA la sivyo nchi hizo zipoteze maslahi yao ya kibiashara na kiuchumi kufuatia kukaa kwao kimya kuhusu matakwa ya Marekani dhidi ya Tehran. Si tu kuwa msimamo wa nchi za Ulaya katika uga wa kimataifa utaingia dosari iwapo makubaliano ya JCPOA yatafutwa, bali itibari ya nchi hizo itakuwa mashakani zikiwa kama pande kuu husika katika mazungumzo hayo ya nyuklia. Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa makubaliano ya JCPOA yalikuwa yenye mafanikio na kwamba Umoja huo una azma thabiti ya kuyalinda. Hakuna nchi inayoweza kuyafuta makubaoiano hayo kwa upande mmoja kwa sababu makubaliano hayo si makubaliano ya pande mbili pekee bali ni urithi wa kimataifa. 

Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya 

Wakati huo huo Brussels imetoa radiamali hasi kuhusu uamuzi wa Trump wa kujitoa katika makubaliano ya JCPOA na kusisitiza kuwa  kuna udharura wa kuyalinda makubaliano hayo na kuendelea kudumisha hali ya usalama barani Ulaya, katika eneo na ulimwenguni kwa ujumla. Sababu hii imeifanya Ulaya ipiganie maslahi yake yenyewe. Huenda masuala hayo yote ndiyo yamempelekea Bruno Le Maire Waziri wa Fedha wa Ufaransa autake Umoja wa Ulaya uchukue msimamo mkali mkabala na Marekani kuhusu hatua yake ya kujitoa katika makubaliano ya JCPOA. Kwa utaratibu huo, inatazamiwa kwamba serikali za Ulaya zitachukua msimamo mkali na wa wazi kuhusu matakwa na vitisho vya vikwazo vya Marekani.   

Bruno Le Maire, Waziri wa Fedha wa Ufaransa