India: Hatutafuata agizo la Marekani la kuiwekea vikwazo Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45118-india_hatutafuata_agizo_la_marekani_la_kuiwekea_vikwazo_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa India amesema kuwa, nchi yake haitofuata maagizo ya Marekani ya kuiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 29, 2018 03:12 UTC
  • India: Hatutafuata agizo la Marekani la kuiwekea vikwazo Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa India amesema kuwa, nchi yake haitofuata maagizo ya Marekani ya kuiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Sushma Swaraj, aliyasema hayo mjini New Delhi Jumatatu ya jana katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kwamba India itaendeleza mashirikiano ya kibiashara na Iran licha ya vikwazo vya Marekani dhidi ya mashirika mbalimbali ya Iran.

Sushma Swaraj kulia, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa India amefafanua kuwa, hakuna nchi yenye uwezo wa kuipangia New Delhi maamuzi yake kama ambavyo nchi hiyo haikubali kushinikizwa na upande wowote. Kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na India kuanzia 2016 na 2017 kilipanda na kufikia Dola bilioni 12 na milioni 900.

Donald Trump, kiongozi asiyesikiliza ushauri kutoka kwa yeyote na anayeendelea kupingwa duniani

Hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani sambamba na kutoheshimu makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya Iran alitangaza kuiondoa nchi yake katika mapatano hayo maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), huku nchi nyingine kama Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambazo ni wahusika katika makubaliano tajwa zikitangaza kuendelea kuyaheshimu. Weledi wa mambo wanaamini kuwa hatua za upande mmoja zinazochukuliwa na rais wa Marekani zitapelekea kutengwa nchi hiyo kimataifa.