Jul 01, 2018 07:46 UTC
  • Matarajio ya Bangladesh kwa China kuhusu wakimbizi Waislamu wa Myanmar

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China ameeleza utayari wa serikali ya Myanmar kwa ajili ya kurejea nchini humo mamia ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya kutoka Bangladesh.

Wang Yi amesema hayo katika mazungumzo yake mjini Beijing na Abul Hassan Mahmud Ali, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bangladesh na kueleza kuwa, wamepokea taarifa kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu wa Myanmar inayoeleza utayari wa nchi hiyo kwa ajili ya kurejea wakimbizi wa Myanmar kutoka Bangladesh. China ni muungaji mkono mkuu wa serikali ya Myanmar na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana serikali ya Bangladesh inataraji kuiona Beijing ikifanya juhudi maradufu na kuwa na nafasi athirifu kieneo na kimataifa kwa minajili ya kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili wakimbizi Waislamu Warohingya.

Bangladesh ina wakimbizi Waislamu takribani milioni moja kutoka jamii ya Rohingya nchini Myanmar ambao wamekimbilia katika nchi hiyo jirani kutokana na maudhi, mateso na hata mauaji dhidi yao yanayofanywa na jeshi na Mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka. Filihali wakimbizi hao wanakabiliwa na hali mbaya kutokana na kuishi katika mazingira mabovu katika kambi za wakimbizi.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bangladesh na China

Kuzuka matatizo ya kiusalama, kiuchumi, kijamii, kiafya, kitiba na kutokuwa na uwezo serikali ya Dhaka wa kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo, ni jambo ambalo limeisukuma serikali ya Bangladesh na kuifanya katika siku za hivi karibuni izidishe mazungumzo yenye lengo la kuandaa mazingira ya kurejea wakimbizi hao Waislamu katika nchi yao.

Kuhusiana na jambo hilo, tayari serikali ya Bangladesh imetiliana saini makubaliano na serikali ya Myanmar na Umoja wa Mataifa lakini hadi sasa makubaliano hayo hayajapelekea kupatiwa ufumbuzi matatizo ya Waislamu hao. Serikali ya China nayo ambayo ni muungaji mkono mkuu wa serikali ya Myanmar hadi sasa haijachukua msimamo na hatua ambayo imesaidia kutatuliwa matatizo ya Waislamu Warohingya. Pamoja na hayo, Bangladesh inaamini kuwa, endapo China itatumia nafasi muhimu iliyonayo inaweza kusaidia kupatiwa ufumbuzi mgogoro huo wa kieneo na hivyo kujiongezea itibari yake kimataifa. 

Waislamu wa Rohingya 

Profesa William Orman Beeman mtaalamu wa masuala ya kisiasa anaamini kuwa: Madola yenye nguvu kieneo na kimataifa yanajifanya kuwa, Myanmar haina faida wala maslahi ya kiistratejia kwao. Hii ni katika hali ambayo, baadhi ya nchi jirani zimekuwa zikinufaika na kugunduliwa nishati ya mafuta kwa mara ya kwanza nchini humo. Vitendo vya kinyama vya keshi la Myanmar dhidi ya Waislamu Warohingya ni jambo ambalo limewatia wasiwasi mkubwa watu wote wanaoguswa na suala la haki za binadamu katika maeneo mbalimbali duniani. Hata hivyo inaonekana kuwa, vitendo hivyo vya kinyama bado havijayafanya baadhi ya madola makubwa duniani yachukue hatua ya kukabiliana na ukiukaji huo wa haki za binadamu.

China na Myanmar zina mpaka wa pamoja wenye urefu wa kilomita 2000 na Beijing imekuwa na nafasi muhimu katika mipango ya ustawi wa kiuchumi ya jirani yake huyo na ushirikiano wa nchi hizo katika sekta ya nishati ndio kiwango cha juu kabisa cha ushirikiano wa pande mbili.

Pamoja na hayo kwa mtazamo wa Bangladesh ni kuwa, serikali ya China inapaswa kubeba majukumu zaidi sambamba na kutanguliza mbele maslahi ya umma katika eneo na hivyo kusaidia kurejesha amani na uthabiti. Kwani kinyume na hivyo, kuendelea mgogoro wa Myanmar kunaweza kutishia usalama katika mipaka ya nchi hiyo.

Waislamu wa Rohingya wakiyahama makazi yao

Moja ya matarajio ya Waislamu wa jamii ya Rohinga  kwa China ni kuilazimisha serikali ya Myanmar ikubali haki ya uraia ya Waislamu hao na kwa muktadha huo matatizo yao yawe yamepatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Alaa kulli haal, safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bangladesh nchini China inaonyesha kuwa, serikali ya Dhaka haijakata tamaa na hatua yoyote ile ya serikali ya Myanmar pamoja na nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Waislamu wa Myanmar na inataraji kuiona serikali ya Beijing ikiingia uwanjani na kuchukua hatua za kutatua matatizo ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Tags