Bunge la Israel lapasisha sheria ya ubaguzi, Wabunge Waarabu wahamaki
Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) limeupasisha muswada wa sheria inayotaka kutambuliwa Israel kama 'dola la Mayahudi pekee' licha ya upinzani mkali na malalamiko kutoka kila pembe ya dunia.
Muswada huo umepasishwa leo Alkhamisi kwa kura 62 dhidi ya 55, baada ya mjadala mkali ndani ya bunge hilo na licha ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kufanya maandamano nje ya bunge hilo wakiipinga sheria hiyo.
Akizungumza muda mfupi baada ya kupasishwa sheria hiyo tata, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjami Netanyahu ametaja kitendo cha kupasishwa sheria hiyo kama nukta muhimu kwenye historia ya Uzayuni.
Wabunge wenye asili ya Kiarabu katika Bunge la Knesset wamehamakishwa na kupasishwa sheria hiyo, ambapo mbali na kuchana nakala zake, wamesikika wakifoka wakisema "Netanyahu umepasisha sheria ya apartheid, umapasisha sheria ya ubaguzi, kwa nini unakiogopa Kiarabu?"
Mbali na sheria hiyo kuzifadhilisha 'thamani za Kizayuni' badala ya 'thamani za kidemokrasia' katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel, lakini pia inautambua Quds kama mji mkuu wa Israel, sanjari na kukitambua Kiebrania kama lugha rasmi na kukitweza Kiarabu.
Watu zaidi ya elfu saba walifanya maandamano katika barabara za mji wa Tel Aviv siku chache zilizopita, kupinga sheria hiyo ya kibaguzi ya utawala haramu wa Israel, ambayo makundi ya kiraia yameitaja kama sheria ya 'apartheid'.