Jul 20, 2018 07:41 UTC
  • Mpango wa jeshi la Myanmar wa kuwaua Waislamu wa Rohingya

Shirika la kutetea haki za binadamu la eneo la Asia, limetangaza kwamba ukatili na mauaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya yaliyofanywa na jeshi la Myanmar yaliratibiwa mapema na kutekelezwa kwa mpangilio maalumu.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo lenye makao yake nchini Thailand imesema kwamba, kabla ya kuanzisha mashambulizi dhidi ya Waislamu wa Rohingya, jeshi la Myanmar lilianza kudhibiti nyenzo zao za kujilinda na mkabala wake likaanza kuwapatia raia wa kawaida silaha na mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kuwashambulia Waislamu hao. Kadhalika ripoti hiyo imeongeza kwamba, kabla ya kuanza mauaji hayo dhidi ya Waislamu, serikali ilizuia vyakula kuingizwa katika mkoa wa Rakhine. 

Shirika la Haki za Binaadamu la Fortify Rights la Asia

Shirika la Haki za Binaadamu la Fortify Rights la Asia limelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwasilisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC suala la mauaji dhidi ya Waislamu wa Myanmar  ambayo yalitekelezwa chini ya usimamizi wa makamanda na viongozi wa polisi 22 wa nchi hiyo. Tangu mwezi Agosti mwaka jana na kwa kisingizio cha kupambana na wanamgambo wenye silaha, jeshi la Myanmar lilianzisha mauaji makubwa na jinai mbalimbali dhidi ya jamii ya Waislamu wa eneo la magharibi mwa nchi hiyo. Katika mashambulizi hayo, maelfu ya Waislamu wa Rohingya waliuawa, wanawake kubakwa na kudhalilishwa kijinsia, vijiji karibu 200 kuchomwa moto na Waislamu wengine karibu milioni moja kulazimika kuishi kama wakimbizi nje ya nchi hiyo.

Tags