Waislamu Warohingya wanauawa kwa umati na kubakwa Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46918-waislamu_warohingya_wanauawa_kwa_umati_na_kubakwa_myanmar
Shirika moja la kimataifa la madaktari wataalamu limesema limekusanya ushahidi unaoonyesha wazi kuwa Waislamu Warohingya wanauawa kwa umati na kubakwa nchini Myanmar.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jul 21, 2018 02:57 UTC
  • Waislamu Warohingya wanauawa kwa umati na kubakwa Myanmar

Shirika moja la kimataifa la madaktari wataalamu limesema limekusanya ushahidi unaoonyesha wazi kuwa Waislamu Warohingya wanauawa kwa umati na kubakwa nchini Myanmar.

Ripoti iliyotangazwa Ijumaa na Madaktari Watetezi wa Haki za Binadamu (PHR) inaonyesha kuwa Waislamu wamekuwa wakipigwa risasi, kukatwa kwa mapanga au kuuawa kwa mabomu. Taarifa hizo zimekusanywa kutoka kwa wakimbizi Warohingya ambao wamekimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Ripoti nyingine iliyotangazwa Alhamisi na shirika la kutetea haki za binadamu la Fortify Rights imesema Jeshi la Myanmar lilipanga na kutekeleza kwa makusudi mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu Warohingya katika jimbo la Rakhine magharibi mwa nchi hiyo. Ripoti hiyo imesema wimbi jipya la maangamizi ya umati ya Waislamu Warohingya lililoanzishwa na jeshi Agosti mwaka jana ni jinai iliyopangwa na kuratibiwa kwa malengo maalumu. Ripoti hiyo imesema madai kuwa hujuma ya waasi ndiyo iliyopelekea kuanza oparesheni dhidi ya Waislamu ni kisingizio tu kwani mauaji hayo yalipangwa kwa miezi kadhaa kabla ya tukio hilo.

Mazishi ya Mwislamu Mrohingya

Wimbi jipya la jinai dhidi ya Waislamu Rarohingya zilishika kasi tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka jana. Hadii sasa  jinai hizo zimepelekea kuuliwa Waislamu karibu elfu 10 na kujeruhiwa makumi ya maelfu ya wengine huku wengine karibu laki nane wakilazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Zeid Ra'ad Al Hussein anasisitiza kwamba, kuna udharura wa kufika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kufanya uchunguzi kuhusu ukatili unaofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu.