Trump atilia shaka ripoti ya CIA kuhusu mauaji ya Khashoggi
(last modified Sun, 18 Nov 2018 14:09:48 GMT )
Nov 18, 2018 14:09 UTC
  • Trump atilia shaka ripoti ya CIA kuhusu mauaji ya Khashoggi

Rais Donald Trump ametilia shaka ripoti iliyovuja ya Shirika la Ujasusi la Marekani CIA kwamba Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman aliamuru mauaji ya mpinzani wa utawala huo wa kifalme, Jamal Khashoggi.

Trump amesema ni mapema mno kuhukumu kuwa Bin Salman alitoa amri ya kuuawa Khashoggi. Hata hivyo katika kile kinachoonekana ni kujikanganya, Trump amesema, "Mauaji ya Khashoggi hayakupaswa kufanyika, na huenda ripoti ya CIA kuwa Bin Salman alitoa agizo la kufanyika mauaji hayo ina ukweli, lakini tusubiri ripoti kamili siku ya Jumanne."

Hii ni katika hali ambayo, siku chache zilizopita, duru za kuaminika zililiambia gazeti la Washington Post kwamba, shirika CIA limefikia natija kwamba, Muhammad bin Salman ndiye aliyetoa amri ya kuuliwa Jamal Khashoggi ambaye alikuwa mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia. 

Trump amekuwa akiukingia kifua utawala wa Aal-Saud wazi wazi

Washington Post imefichua kwamba, mazungumzo ya simu ya balozi na mwanamfalme wa Aal-Saud Khalid bin Salman na Khashoggi na kutakiwa mwanahabari huyo kwenda kwenye ubalozi wa Saudia mjini Istanbul vilifanyika kwa amri ya Muhammad bin Salman.

Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari aliyekuwa mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, aliuliwa  kikatili kwenye ubalozi mdogo wa Uturuki mjini Istanbul, tarehe Pili mwezi uliopita wa Oktoba.