Russia yaamua kususia mkutano wa Marekani wa Warsaw
Ikiwa ni katika fremu ya malengo yake inayoyafuatilia katika eneo la Mashariki ya Kati, Marekani ina mpango wa kuitisha mkutano hapo tarehe 13 na 14 mwezi ujao wa Februari huko Warsaw mji mkuu wa Poland chini ya anwani ya "Mkutano wa Amani na Usalama katika Mashariki ya Kati".
Washington inadai kuwa imezialika nchi 70 kuhudhuria mkutano huo ambao utafanyika katika ngazi ya Mawaziri wa Mambo ya Nje. Hata hivyo baadhi ya nchi zimetangaza kuwa hazitashiriki katika mkutano huo. Kwa sasa Russia inatambulika kama moja ya nchi zenye nafasi muhimu katika eneo la Mashariki ya Kati na ni mwanachama wa kundi la 4+1. Vilevile ni wazi kuwa bila ya kuwepo nchi hiyo Washington haiwezi kutoa madai ya kuwepo mwafaka wa kimataifa kuhusu yale yatakayojadliwa katika kikao cha Warsaw likiwemo suala la kukabiliana na siasa na ushawishi wa Iran katika eneo hili. Moscow imekuwa na msimamo hasi katika uwanja huo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Jumanne wiki hii ilitangaza kuwa, Moscow haitashiriki katika mkutano uliodhidi ya Iran uliopangwa kufanyika Warsaw nchini Poland. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeeleza kuwa: Mkutano wa Warsaw utatafanyika kwa lengo la kutoa pigo kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo yamepasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na Iran, Russia, China na Troika ya Umoja wa Ulaya zinataka kulindwa makubaliano hayo ya kimataifa.
Moscow inaona kuwa, mkutano unalenga makubaliano ya JCPOA na kama alivyotilia mkazo Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, umeitishwa kwa lengo la kukabiliana na ushawishi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati. Viongozi wa Marekani wanadhani kwamba, kupitia mikutano kama huu wataweza kuzishawishi nchi kadhaa na kuzivutia upande wa serikali ya Washington na hivyo kuanzisha aina fulani ya muungano wa kimataifa dhidi ya Iran.
Akizungumza Jumanne wiki hii kwa njia ya video katika Mkutano wa Uchumi wa Davos, Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwa mara nyingine tena aliitaja Iran kuwa tishio na kwamba ni chanzo cha ukosefu wa amani katika eneo hili. Pompeo alisema kuwa, anataraji kwamba Washington itafanikiwa kuanzisha muungano wa kikanda dhidi ya Iran. Pamoja na hayo ushahidi unaonyesha kuwa, madola makubwa duniani hususan nchi wanachama wa kundi la 4+1 zina msimamo hasi kuhusiana na suala hilo na wala hazina azma ya kuunga mkono msimamo huo wa Washington wa kupinga makubaliano ya JCPOA.
Russia kwa upande wake inaona kuwa, malengo ya Washington na Tel Aviv ni kuhakikisha kwamba, matokeo ya mkutano huo yanakuwa dhidi ya Iran na kwa njia hiyo Marekani sambamba na kutumia nguvu ya kiuchumi na kuzidisha mashiniko kwa Iran, iweze pia kustafidi na nguvu laini yaani vita vya kipropaganda na kisiasa kwa ajili ya kuzuia ushawishi wa Iran katika Mashariki ya Kati.
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia Jumanne wiki hii aliutaja mkutano unaopangwa kufanywa na Marekani hum Warsaw kuwa ni miongoni mwa mikusanyiko uliyo dhidi ya Iran na kwamba kikao hicho ni haribifu kwa usalama wa eneo la Mashariki ya Kati. Ni dhahir shahir kuwa katika kipindi cha sasa lengo kuu la Marekani ni kuilazimisha Iran kuondoka huko Syria, suala ambalo lilisisitizwa pia huko nyuma na baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa serikali ya Washington kama John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa serikali ya nchi hiyo.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema, lengo jingine la kuitishwa mkutano wha Warsaw ni kutaka kusambaratisha jitihada za jamii ya kimataifa za kurejesha amani na utulivu katika Mashariki ya Kati. Taarifa hiyo iliongeza kuwa: Masuala muhimu ikiwemo kadhia ya Palestina haijaashiriwa katika ajenda ya mkutano huo.
Ni wazi kuwa serikali ya Trump imeazimia kukibadili kikao hicho cha Warsaw na kuwa mkutano wa nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel katika fremu ya siasa zake kuhusu eneo la Mashariki ya Kati ambazo moja ya misingi yake mikuu ni kuasisi muungano wa kieneo kwa kuwashirikisha waitifaki wake wa Kiarabu na utawala huo haramu na kwa utaratibu huo kadhia ya Palestina iwekwe kando, na Iran na siasa zake katika eneo hili ziarifishwe kama tatizo kuu la Mashariki ya Kati.
Wakati huo huo, Washington kwa upande mwingine inataka kutekeleza mpango uliopewa jina la "Muamala wa Karne" eti wenye lengo la kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina na inadhani kwamba, kuitishwa mkutano wa Warsaw ambao serikali ya Trump imedai kuwa utafanyika kwa ajili ya amani ya Mashariki ya Kati, ni fursa nzuri kwa ajili ya kupata uungaji mkono wa Waarabu kuhusu mpango huo.