Mwakilishi wa Trump: Hatuna ratiba yoyote ya kuanzisha vita na Iran
Mwakilishi wa serikali ya Marekani katika masuala ya Iran sambamba na kutoa tuhuma zao za kila siku dhidi ya Tehran amesema kuwa, nchi yake haina ratiba yoyote ya kuanzisha vita dhidi ya Iran.
Brian Hook alitoa kauli hiyo jana Jumatano wakati alipohojiwa na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar na kusema kuwa "sisi hatupangi kuanzisha vita dhidi ya Iran."
Mkuu huyo wa genge la kuchukua hatua dhidi ya Iran katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani vile vile amedai kuwa, kujitoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA kumeipa nchi hiyo uhuru wa kuishinikiza inavyopenda Tehran.
Mwakilishi huyo wa rais wa Marekani katika masuala ya Iran pia amewashukuru washiriki wa kikao cha Warsaw hususan nchi za Ulaya.
Matamshi hayo ya Brian Hook yametolewa katika hali ambayo, gazeti la The Guardian linalochapishwa mjini London Uingereza limesema katika ripoti yake kwamba nchi muhimu za Ulaya zimekipuuza kikao hicho cha Warsaw kwa kupeleka wajumbe wa ngazi za chini kushiriki kwenye kikao hicho.
Kikao cha siku mbili kilichoitishwa na Marekani kwa ajili ya kuipiga vita Iran kilianza jana Jumatano katika mji mkuu wa Poland, Warsaw.
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia mazingira yaliyotawala maandalizi ya kikao hicho cha Warsaw na kususiwa na nchi za duniani akisema: "kikao hicho kimefeli hata kabla ya kuanza kwake."