Kufeli mkutano wa Warsaw
-
Mike Pompeo
Baada ya propaganda kubwa za wiki kadhaa zilizofanywa na Marekani kuhusu mkutano uliokuwa dhidi ya Iran wa Warsaw nchini Poland, hatimaye mkutao huo wa siku mbili ulimaliza kazi zake jana Alkhamisi bila ya mafanikio.
Ajenda iliyokuwa imetangazwa ya mkutano huo ilikuwa "Amani na Usalama Mashariki ya Kati" lakini maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo walikuwa wamesisitiza kuwa, mkutano huo utajikiza zaidi juu ya Iran na ushawishi wa nchi hiyo katika eneo la Mashariki ya Kati. Hata hivyo kutokana na nchi nyingi kukataa kushirikiana na serikali ya Marekani katika sera zake za kuipiga vita Jamhuri ya Kiislamu, taarifa ya mwisho ya mkutano huo imejiepusha kutaja nchi maalumu.
Wakati huo huo katika mazungumzo yao na waandishi habari baada ya mkutano wa Warsaw, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na Poland ambao walikuwa wenyeji wa mkutano huo wameitaja Iran kuwa ni "tishio la usalama". Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amedai kuwa, mkutano huo ni wa kihistoria kwa kuwakutanisha katika chumba kimoja viongozi wa Israel na nchi za Kiarabu ambao wamezungumzia kuhusu "hatari ya Iran". Pompeo amesema: "Nchi zote washiriki hazijahitilafiana kuhusiana na suala kwamba, Iran ni hatari na sasa Marekani inataka kuweka vikwazo na mashinikizo zaidi dhidi ya serikali ya Iran."
Hii ina maana kwamba, ili kuthibitisha madai yake dhidi ya Iran, Mike Pompeo ameashiria waitifaki wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati kama Israel na baadhi ya tawala za Kiarabu kama Saudi Arabia ambazo kimsingi ni maadui wa siku nyingi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; hivyo sisitizo la serikali ya Washington katika mkutano wa Warsaw kwamba, eti "Iran ni tishio la usalama na amani", halina maana yoyote. Hii ni pamoja na kuwa Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani hakuashiria kwa makusudi nchi kubwa na zenye taathira katika masuala ya kimataifa kama wanachama wa kundi la 4+1 yaani Uingereza, Ufaransa, Russia, China na Ujerumani ambazo zimepinga misimamo ya Marekani dhidi ya Iran au nchi kama Russia ambayo hazikushiriki kabisa katika mkutano wa Warsaw au zile zilizutuma ujumbe wa ngazi za chini.
Wakati huo huo matamshi yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence pambizoni mwa mkutano wa Warsaw ambaye amethibitisha kwamba, kuna hitilafu baina ya Marekani na Ulaya kuhusiana na kadhia ya Iran, ni kielelezo kwamba, Umoja wa Ulaya na nchi kubwa za bara hilo zimepuuza misimamo ya Washington dhidi ya Iran na zinaendelea kupinga matakwa ya Marekani ya kutupiliwa mbali makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Pance ameitaja Iran kuwa ni “tishio kubwa zaidi la amani” na amezitaka nchi za Ulaya zijiondoe katika makubaliano ya nyuklia ya nchi hizo na Jamhuri ya Kiislamu. Vilevile ameitaja hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuanzisha mfumo wa mabadilishano ya kibiashara na kifedha na Iran kuwa inakusudia kuvunja vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Ombi hilo la Mike Pence likepingwa na kukataliwa na Umoja wa Ulaya.
Niels Annen ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema kuwa: "Jibu letu ni jepesi sana. Ulaya inapiga hatua kwa tahadhari na kwa pamoja Tumefanya mahesabu kuhusiana na vikwazo na mazungumzo na Ulaya itaendelea kushikamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.”
Kwa msingi huo licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na Marekani kutayarisha mkutano wa Warsaw na kutaka kuunda muungano wa kimataifa dhidi ya Iran, lakini hatua ya washiriki mkutano huo ya kukataa matakwa ya Marekani na Poland ya kutoa taarifa ya pamoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ni pigo kubwa na kielelezo cha kufeli mkutano huo.
Ni kwa kutilia maanani hayo ndiyo maana msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, Bahram Qassemi amasema: “Mkutano wa Warsaw ulishindwa hata kabla ya kuanza kwake na taarifa yake ya mwisho ni waraka usio na maana uliotayarishwa na kutolewa na nchi mbili zilizosimamia mkutano huo na wala hauna hadhi yoyote.”