Guterres: Kuna udharura wa kupambana na chuki dhidi ya Uislamu duniani
Katibu MKuu wa Umoja wa Mataifa sanjari na kulaani mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya misikiti miwili katika mji wa Christchurch nchini New Zealand jana Ijumaa na kuua makumi ya watu, ametoa mwito wa kuundwa mikakati ya kupambana na chuki dhidi Uislamu zinazoenea kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya dunia.
Kupitia msemaji wake, Antonio Gueterres, Katibu Mkuu wa UN ameeleza kushtushwa kwake na ukatili huo wa jana katika misikiti ya New Zealand. Taarifa hiyo ya Antonio Guterres imeongeza kuwa, kuenezwa propaganda chafu na kuchafuliwa Uislamu ni katika mambo yaliyochochea mashambulio hayo ya jana ya kigaidi. Guterres amesema kuna udharura wa kufanya jitihada za pamoja za kupambana na uenezaji wa chuki dhidi ya Uislamu duniani.

Gaidi mwenye umri wa miaka 28 kwa jina Brenton Tarrant raia wa Australia ambaye alihusika katika shambulizi dhidi ya msikiti mmoja kati ya miwili iliyoshambuliwa nchini New Zealand amekuwa akijitangaza kuwa ni mfuasi wa sera za kibaguzi za Rais Donald Trump wa Marekani. Magaidi waliobeba bunduki za otomatiki walishambulia misikiti miwili ya Al Noor na Linwood katika mji wa Christchurch wakati wa Swala ya Ijumaa, ambapo watu wasiopungua 49 wakiwemo wanawake na watoto wadogo waliuawa na wengine wengi wamejeruhiwa.