OPEC: Ni muhali kuyaondoa mafuta ya Iran katika soko la dunia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53230-opec_ni_muhali_kuyaondoa_mafuta_ya_iran_katika_soko_la_dunia
Katibu Mkuu wa Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) amesema ni muhali kuyaondoa mafuta ya Iran katika soko la kimataifa na kwamba shirika hilo linafanya juu chini kuhakikisha kuwa siasa haziingizwi katika biashara ya mafuta.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 02, 2019 09:10 UTC
  • OPEC: Ni muhali kuyaondoa mafuta ya Iran katika soko la dunia

Katibu Mkuu wa Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) amesema ni muhali kuyaondoa mafuta ya Iran katika soko la kimataifa na kwamba shirika hilo linafanya juu chini kuhakikisha kuwa siasa haziingizwi katika biashara ya mafuta.

Mohammad Barkindo ameyasema hayo katika Maonyesho ya Gesi na Mafuta yanayofanyika hapa Tehran na kubainisha kuwa, kimsingi ni jambo lisilowezekana kuyaondoa mafuta ya Iran katika soko la dunia na kwamba kile kinachofanyika Iran, Venezuela na Libya kitakuwa na taathira hasi katika soko la mafuta na nishati duniani.

Ameongeza kuwa, "Tumekuwa na changamoto nyingi katika kipindi cha miaka 60 iliyopita ndani ya OPEC, lakini changamoto hizo tukazipatia ufumbuzi kwa ushirikiano."

Katibu Mkuu wa OPEC ameyaunga mkono matamshi ya Waziri wa Mafuta wa Iran, Bija Zanganeh aliyesema jana kuwa, nchi zinazotumia mafuta kama silaha zitaliangusha Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani.

Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani 

Haya yanajiri siku chache baada ya Emmanuel Ibe Kachikwu, Waziri wa Mafuta wa Nigeria kutoa radiamali kufuatia uamuzi wa Marekani wa kufuta kibali cha ununuzi wa mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, ni jambo lisilowezekana kufikisha mauzo ya mafuta ya Iran kwenye kiwango cha sifuri.

Aprili 22, Ikulu ya Marekani (White House) iliziagiza nchi nane ambazo zilikuwa zimeruhusiwa na Washington kuendelea kununua mafuta ya Iran licha ya vikwazo vya US ziache kuagiza bidhaa hiyo kuanzia Mei Mosi (jana Jumatano), vinginevyo zitawekewa vikwazo.