Zarif akimhutubu Trump; Kiongozi Muadhamu ameshatangaza silaha za nyuklia ni haramu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53760-zarif_akimhutubu_trump_kiongozi_muadhamu_ameshatangaza_silaha_za_nyuklia_ni_haramu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatatu usiku amejibu madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kuwa eti Iran inafuatilia silaha za nyuklia na kusema, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshatangaza kuwa silaha za nyuklia ni haramu.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
May 28, 2019 03:31 UTC
  • Zarif akimhutubu Trump; Kiongozi Muadhamu ameshatangaza silaha za nyuklia ni haramu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatatu usiku amejibu madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kuwa eti Iran inafuatilia silaha za nyuklia na kusema, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshatangaza kuwa silaha za nyuklia ni haramu.

Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mohammad Javad Zarif, ameandika kuwa Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameshatoa fatwa ya kuharamisha silaha za nyuklia na kutangaza kuwa Iran haifuatilii silaha za nyuklia.

Zarif ameendelea kwa kuandika kuwa, ugaidi wa kiuchumi wa Timu B umewadhuru  watu wa Iran na kuibua taharuki katika eneo la Asia Magharibi. Aidha amesema hatua za kivitendo na si maneno ya Donald Trump ndizo zitakazoonyesha iwapo anafuatilia lengo hilo la Timu B au lengo jingine.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema timu "B" inayoundwa na John Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa rais wa Marekani, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na Bin Zayed mrithi wa kiti cha ufalme wa Imarati (UAE) wanajaribu kuisukuma Marekani kuanzisha vita vya kijeshi dhidi ya Iran.

Siku ya Jumatatu, Rais Trump akizungumza na waandishi mjini Tokyo akiwa ameandamana na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe alikariri tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran kwa kudai kuwa lengo pekee la mashinikizo ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuizuia kumiliki silaha za nyuklia. Rais wa Marekani aliendelea kutoa matamshi ya kichekesho na kudai kuwa anataka ustawi wa kiuchumi nchini Iran. Madai ya Trump yanatolewa katika hali ambayo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umeshatoa ripoti 14 hadi sasa ambazo zimethibitisha kuwa, shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani. Aidha wakala huo wa nyuklia wa Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa Iran inatekeleza ahadi zake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Marekani ilichukua uamuzi wa upande moja na kujiondoa katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei 8 mwaka 2018 sambamba na kurejesha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran. Hatua hiyo ya Trump imelaaniwa vikali kimataifa na uungaji mkono pekee aliopata ni kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi ya kimsingi katika kukabiliana na mhimili wa Marekani, Saudia na Utawala wa Kizayuni.