Ujumbe unaokinzana wa Trump kwa Iran
(last modified Fri, 31 May 2019 02:22:54 GMT )
May 31, 2019 02:22 UTC
  • Ujumbe unaokinzana wa Trump kwa Iran

Rais Donald Trump wa Marekani siku zote amekuwa na misimamo ya kihasama na kiadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na daima anasisitiza suala la kuzidisha masihinizo dhidi ya Tehran kwa shabaha ya kuilazimisha kukubali matakwa ya Washington.

Pamoja na hayo misimamo hiyo hasi haikuwa na matunda yaliyokusudiwa, kinyume kabisa na matarajio ya serikali ya Trump. Kwa msingi huo hivi sasa kuna ishara kwamba Marekani inajitayarisha kufanya mazungumzo na Iran. Miongoni mwa ishara hizo ni kwamba, Trump mbali na kutangaza kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo na Tehran, amesema kuwa, ameipatia Uswisi ambayo inalinda maslahi ya Marekani nchini Iran, nambari makhsusi ya simu ili viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu wawasiliane naye. Katika safari yake ya hivi karibuni nchini Japan pia Donald Trump alikaribisha upatanishi wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Shinzō Abe baina ya Marekani na Iran na vilevile safari yake tarajiwa mjini Tehran. 

Pamoja na misimamo na hatua hizo, Washington inaendelea kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran, kueneza propaganda chafu na kuzitaka nchi za Kiarabu zishikamane kwa ajili ya kukabiliana na kile alichodai ni vitisho vya Iran. Kwa utaratibu huo serikali ya Trump inatekeleza kwa pamoja siasa na sera za kuzidisha mashinikizo na wakati huo huo kutoa wito wa kufanya mazungumzo na Iran. 

Donald Trump

Katika uwanja huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Morgan Ortagus amesema nchi yake itaendelea kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran ili iilazimishe Tehran kuketi kwenye meza ya mazungumzo na serikali ya Washington. Ortagus amedai katika mkutano wa waandishi habari kwamba: "Tutazidisha mashinikizo dhidi ya Iran na kuilazimisha nchi hiyo kufanya mazungumzo ya kufikia mapatano mapya." Baada ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani ilianzisha vita vya pande zote vya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Washington inadai kuwa, lengo la mashinikizo hayo ni kufikia makubaliano mapya na Tehran ambayo yatahusu masuala yote yanayopewa umuhimu na Marekani. 

Msimamo huu wa Marekani umekosolewa vikali na Russia ambayo ni miongoni mwa madola makubwa yanayopinga sera za kijuba na kibeberu za serikali ya Washington. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov amekosoa vikali misimamo hiyo ya serikali ya Marekani kuhusu Iran na kusema kuwa Washington inataka kuitisha Jamhuri ya Kiislamu. Ryabkov ameliambia gazeti la Rossiyskaya Gazeta kwamba: Kwa sasa tunashuhudia mashinikizo makubwa ya Marekani dhidi ya Iran na jitihada za kutaka kuitishia nchi hiyo. Wakati huo huo hakushuhudiwi ajenda yoyote ya maana kutoka Marekani na wala nchi hiyo haina njia mbadala na imetosheka kwa kutangaza tu kwamba, iko tayari kufanya mazungumzo. Hata hivyo msimamo huu hauwezi kutayarisha uwanja mzuri wa kufanya mazungumzo."

Sergei Ryabkov

Katika mahojiano haya ambayo yamechapishwa mapema leo Alkhamisi, Sergei Ryabkov amesema kuwa, kama kweli Marekani inataka kufanya mazungumzo na kuwa na uhusiano na Iran inapaswa kutangaza itafanya nini mkabala wa uamuzi wowote wa Iran wa kushiriki katika mazungumzo kama hayo. 

Ni kutokana na misimamo hii ya kiuadui na kihasama ya Marekani na kutoaminika kwake ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei akakataza aina yoyote ya mazungumzo baina ya Iran na Marekani. Akihutubia hadhara ya wahadhiri wa vyuo vikuu alasiri ya Jumatano ya jana, Ayatullah Ali Khamenei aliyataja mazungumzo kuwa ni mbinu inayotumiwa na Marekani kwa ajili ya kukamilisha stratijia ya mashinikizo dhidi ya Iran.

Ayatullah Ali Khamenei

Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitafanya mazungumzo na Marekani na kusema: "Kama nilivyowahi kusema huko nyuma, hatutafanya mazungumzo na Marekani kwa sababu kwanza, mazungumzo hayo hayana faida, na pili yana madhara." Vilevile katika hotuba yake ya tarehe 14 Mei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema: "Chaguo la taifa la Iran ni kusimama kidete dhidi ya Marekani, na katika mpambano huo Marekani italazimika kulegeza kamba na kurudi nyuma." 

Tags