Waziri Mkuu wa Pakistan: Umma upambane na chuki dhidi ya Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53852-waziri_mkuu_wa_pakistan_umma_upambane_na_chuki_dhidi_ya_uislamu
Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan ametoa mwito kwa umma wa Kiislamu kupambana na dhulma na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 01, 2019 06:55 UTC
  • Waziri Mkuu wa Pakistan: Umma upambane na chuki dhidi ya Uislamu

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan ametoa mwito kwa umma wa Kiislamu kupambana na dhulma na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu duniani.

Amesema hayo leo Jumamosi kwenye hotuba yake katika Mkutano wa 14 wa Viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Makka nchini Saudi Arabia.

Amefafanua kuwa, "OIC kama taasisi na viongozi wa nchi wanachama wake wana jukumu kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu. Iwapo mtu atamdhalilisha Mtume wetu SAW, OIC inabeba dhima ya kufeli kutoa ufafanuzi kwa mataifa mengine kuhusu mahaba tuliyonayo kwa Mtukufu huyo."

Waziri Mkuu wa Pakistan ameitaka jamii ya kimataifa na hususan nchi za Magharibi kuheshimu hisia za kiroho na kiimani za Waislamu zaidi ya bilioni moja duniani.

Chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi

Amewataka Wamagharibi kutofautisha kati ya 'Uislamu wa wastani' na "Uislamu wa kuchupa mipaka'. Imran Khan ameeleza bayana kuwa, hakuna dini yoyote inayounga mkono ugaidi na misimamo ya kuchupa mipaka na mwa msingi huo Waislamu hawapaswi kulaumiwa kutokana na mashambulizi yote ya kigaidi.

Waziri Mkuu wa Pakistan ameitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kutekeleza wajibu wake katika kulinda haki za Waislamu na kushughulikia vilio vyao.