Pompeo akiri kutotekelezeka mpango wa 'Muamala wa Karne'
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53909-pompeo_akiri_kutotekelezeka_mpango_wa_'muamala_wa_karne'
Licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya kutekeleza mpango wa 'Muamala wa Karne' ambao unalenga kudhamini maslahi ya utawala haramu wa Israel kwa madhara ya Wapalestina, lakini hata Mike Pompeo mwenyewe, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo hana matumaini ya kutekelezwa mpango huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2019 02:42 UTC
  • Pompeo akiri kutotekelezeka mpango wa 'Muamala wa Karne'

Licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya kutekeleza mpango wa 'Muamala wa Karne' ambao unalenga kudhamini maslahi ya utawala haramu wa Israel kwa madhara ya Wapalestina, lakini hata Mike Pompeo mwenyewe, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo hana matumaini ya kutekelezwa mpango huo.

Akizungumza hivi karibuni katika kikao mahususi na cha faragha, Pompeo ametoa matamshi ambayo yanaonyesha kwamba hata mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani mwenyewe hana imani na mpango huo. Kwa mujibu wa faili ya sauti ambayo gazeti la Washington Post imeipata, Pompeo ambaye alikuwa akizungumza katika kikao hicho cha viongozi wa Kiyahudi amesema: Hakuna dhamana yoyote kwamba tutafanikiwa kutatua mzozo wa Israel na Wapalestina. Tunaweza kusema kwamba mpango huu (Muamala wa Karne) takriban hauwezi kutekelezeka na kuna uwezekano usipokelewe vyema.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, serikali ya Trump imekuwa ikifuatilia kwa nguvu zake zote mpango huo na sasa inakaribia kutangaza rasmi utekelezaji wake. Jared Kushner, mshauri na mkwewe Rais Donald Trump wa Marekani siku chache zilizopita alisema kuwa mpango huo unatazamiwa kuzinduliwa rasmi baada ya kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa mujibu wa Usama Hamdan, mkuu wa uhusiano wa kimataifa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, mpango wa 'Muamala wa Karne' unaweza kufupishwa katika anwani mbili kuu, yaani kuongezeka ubeberu na udhibiti wa Marekani katika eneo, juu ya utajiri na vyanzo na vilevile kuufanya utawala ghasibu wa Israel uonekane kuwa utawala wa kawaida kabisa katika eneo na hatimaye kuwekwa pembeni suala la Palestina.

Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani

Kwa mujibu wa mpango huo, utawala ghasibu wa Israel utapewa fursa nyingi mno ambazo hata ziko nje ya mapatano yake ya awali na Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kupata nafasi ya kuyaunganisha maeneo mapya ya Wapalestina unayoyakalia kwa mabavu hivi sasa na yake ya zamani na pia Wapalestina kutakiwa wasahau kabisa suala la kulifanya eneo la Quds Tukufu kuwa mji mkuu wao wakati wa kubuniwa serikali yao huru. Nukta muhimu hapa ni kuwa vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan vitaunganishwa na ardhi nyingine za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa kibaguzi wa Israel na hivyo nchi huru ya baadaye ya Palestina kubanwa katika sehemu ndogo mno kuliko ilivyoainishwa katika mapatano ya huko nyuma. Hii ni pamoja na kuwa nchi hiyo itatakiwa kutokuwa na jeshi. Kwa mujibu wa mpango huo, Wapalestina watatakiwa kufumbia macho haki yao ya kurejea katika ardhi zao za asili, haki ambayo hata azimio nambari 194 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linaitambua rasmi. Trump amemteua mkwewe Kushner kuwa dalali wa kufanikisha mpango huo hatari kwa Wapalestina na umma mzima wa Waislamu.

Wasaliti wa malengo matukufu ya Palestina na Umma wa Kiislamu

Mpango huo unapingwa vikali kutokana na kukiuka wazi mtazamo wa Umoja wa Mataifa na vilevile wanachama wengine wa Kundi la Pande Nne, yaai Umoja wa Ulaya na Russia. Serikali ya Moscow inasema kwamba mpango huo haukubaliki kutokana na kupinga wazi maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa. Hata Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo hadi sasa imetekeleza hatua chungu nzima za mapatano ya ulegezaji msimamo na kufumbia macho maslahi muhimu ya Wapalestina kwa maslahi ya utawala ghasibu wa Israel, inasema kuwa mpango huo haukubaliki hata kidogo. Akizungumza miezi michache iliyopita huko Ramallah kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 54 wa kuasisiwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO, Mahmoud Abbas, mkuu wa malaka hiyo alisema: Kamwe hatutampa Rais Donald Trump wa Marekani ruhusa ya kuuzia utawala wa Israel Quds Tukufu.

Maandamano ya kupinga mpango wa 'Muamala wa Karne'

Hivi sasa katika hatua ya kwanza, serikali ya Trump inapanga kutekeleza hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa mpango huo wa 'Muamala wa Karne' kupitia kikao ambacho imekiandaa huko Manama, mji mkuu wa Bahrain ili iweze kuchangisha fedha za utekelezaji wa mpango huo kutoka kwa nchi na pande zitakazoshiriki katika kikao hicho. Kwa msingi huo Bahrain na Marekai zilitangaza tarehe 19 Mei kwamba kikao hicho cha Manama kitafanyika tarahe 25 na 26 za mwezi huu wa Juni kwa uwenyeji wa nchi mbili hizo na chini ya anwani ya 'Amani kwa ajili ya Machipuo'. Pamoja na hayo lakini kuna shaka kubwa iwapo kikao hicho kitafanikiwa kufikia malengo yake. Washington haujaualika Umoja wa Matifa katika kikao hicho nayo Russia imesema haitashiriki. Kuhusiana na kikao hicho cha Manama Pompeo amesema: Tunataraji nchi za Kiarabu zitashiriki katika kikao hicho ili kwa uchache 'kusikiliza yatakayozungumzwa.' Vilevile amesema hatarajii washiriki wa Kiarabu kutetea kwa nguvu zao zote mpango huo wa Marekani baada ya kumalizika kikao hicho.

Ni kwa kutilia maanani ukweli huo ndipo akabainisha kutokuwa na matumaini juu ya nchi za Kiarabu kupokea vyema kikao hicho.