Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon, Palestina wasusia 'Muamala wa Karne'
Wanazuoni na wasomi wa Kiislamu wa Lebanon na Palestina wamelaani njama ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina iliyopewa jina la 'Muamala wa Karne'.
Wanazuoni hao chini ya Bodi ya Maulamaa wa Kiislamu ya Palestina na Jumuiya ya Wanazuoni wa Lebanon wamekutana katika mji wa Saida nchini Lebanon, ambapo sambamba na kusisitizia udharura wa umoja wa umma wa Kiislamu, wameutaka ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu kutounga mkono mpango huo wa Washington na Tel Aviv wa kuitokomeza kadhia ya Palestina unaotazamiwa kuzinduliwa kesho.
Kadhalika wasomi hao wa Kiislamu wa Lebanon na Palestina wametangaza kuwa suluhu ya mgogoro wa Wapalestina na Israel ni kuruhusiwa wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao za jadi zilizoghusubiwa na Wazayuni.
Haya yanajiri huku maelfu ya wananchi wa Morocco wakifanya maandamano makubwa ya kupinga mkutano huo wa kufungua mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne wa kuangamiza kadhia ya Palestina uliopangwa kufanyika kesho na keshokutwa Jumatano katika mji mkuu wa Bahrain, Manama.
Wakati huohuo, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa mara nyingine amepinga vikali mkutano huo wa Manama na kusema kuwa, mpango wa Marekani wa kuangamiza kadhia ya Palestina utafeli tu.
Tawala vibaraka za Saudi Arabia, Imarati, pamoja na utawala haramu wa Israel zimetangaza kuwa zitatuma wajumbe kwenye mkutano huo wa Manama. Mbali na Iran na Palestina, nchi nyingine zilizotangaza kususia mkutano huo ni Lebanon, Iraq, China na Russia.