Jul 12, 2019 15:18 UTC
  • HRW, Amnesty zataka kufungwa vituo vya kuwazuilia wahajiri Libya

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch, Amnesty International na Baraza la Ulaya la Wakimbizi na Wahajiri (ECRE) yametoa mwito wa kufungwa kambi za kuwazuilia wakimbizi na wahajiri nchini Libya.

Mashirika hayo yanataka kadhia ya wakimbizi na wahajiri wa Libya ipewe kipaumbele katika mkutano ujao wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Ulaya unaotazamiwa kufanyika Julai 15 mjini Brussels.

Taarifa ya leo Ijumaa ya mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu imezitaka nchi za EU kubeba jukumu la kuwapeleka pahali salama wahajiri hao wanaoishi katika hali mbaya nchini Libya, ikiwa ni pamoja na baadhi ya nchi za Ulaya kuwapokea wahajiri hao. 

Kwa mujibu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, watu 5,800 wanapitia kipindi kigumu katika kambi za kuzuilia wahajiri nchini Libya, ambapo 3,800 miongoni mwao wanazuilia karibu na maeneo yanayoshuhudia vita nchini humo.  

 

Baadhi ya wahajiri wanauzwa kama bidhaa sokoni nchini Libya

Haya yanajiri siku chache baada ya makumi ya watu kuuawa katika shambulio la anga lililofanywa na jenerali muasi Khalifa Haftar dhidi ya kituo cha kuhifadhia wahajiri karibu na Tripoli, mji kuu wa Libya.

Kwa mujibu wa Shirika la Wahajiri la Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 1000 wameshauawa tangu jenerali muasi Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati, Marekani na Ufaransa alipoanzisha mashambulio dhidi ya mji kuu wa Libya, Tripoli mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.

Tags