China: Marekani isicheze na moto katika kadhia ya Taiwan
(last modified Fri, 12 Jul 2019 15:38:08 GMT )
Jul 12, 2019 15:38 UTC
  • China: Marekani isicheze na moto katika kadhia ya Taiwan

Waziri wa Mambo ya Nje wa China ameionya vikali Marekani isijaribu kucheza na moto kuhusiana na suala la Taiwan, huku akikosoa vikali mpango wa Washington wa kukiuzia silaha kisiwa hicho ambacho Beijing inasisitiza kuwa ni milki yake.

Wang Yi ametoa indhari hiyo leo Ijumaa katika kikao na waandishi wa habari nchini Hungary na kueleza bayana kuwa, "Hakuna mashinikizo yoyote kutoka nchi ajinabi yanaweza kuzuia kuunganishwa upya eneo la Taiwan na China. Madola ya kigeni hayapaswi kuingilia kati katika suala hili."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa China amesisitiza kuwa, serikali ya Beijing inaiomba Marekani ilichukulie kwa uzito suala la Taiwan na wala isithubutu kucheza na moto katika kadhia hiyo.

Wakati huohuo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Geng Shuang amesema ikilazimu, serikali ya Beijing itayawekea vikwazo mashirika ya Marekani yatakayoiuzia silaha Taiwan.

Haya yanajiri baada ya Marekani kutangaza kuwa itakiuzia kisiwa hicho cha China silaha zenye thamani ya dola bilioni 2.22.

Kutoka kulia, Marais wa China, Marekani na Taiwan

Mpango wa Marekani wa kuiuzia silaha Taiwan ni moja ya mambo ambayo yameibua mivutano kati ya Marekani na China katika miaka ya hivi karibuni. Mwaka jana Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilisema serikali ya Washington imeidhinisha mauzo ya silaha za kijeshi kwa Taiwan yenye thamani ya dola milioni 330.

China inaitambua Taiwan ambayo mwaka 1949 ilijitenga na nchi hiyo baada ya vita vya ndani, kuwa ni sehemu ya ardhi yake.