Maelfu waandamana Uturuki kuilaani Marekani, Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54809-maelfu_waandamana_uturuki_kuilaani_marekani_israel
Maelfu wa wananchi wa mji wa Adana wa kusini mwa Uturuki wamefanya maandamano ya kuilaani Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Jul 16, 2019 22:50 UTC
  • Maelfu waandamana Uturuki kuilaani Marekani, Israel

Maelfu wa wananchi wa mji wa Adana wa kusini mwa Uturuki wamefanya maandamano ya kuilaani Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, waandamanaji hayo walikuwa wanapiga mayowe ya kuilaani Marekani na utawala wa Kizayuni na kusema kuwa tawala hizo ndio wahusika wakuu wa jaribio la mapinduzi ya kijeshi la tarehe 15 Julai 2016 nchini Uturuki.

Waandamanaji hao wameitaka serikali ya Ankara kufunga kambi za kijeshi za NATO nchini mwao hasa kambi ya jeshi la anga ya Incirlik ambayo ilisaidia jaribio hilo lililofeli la mapinduzi.

Serikali ya Uturuki inaamini kuwa, Fethullah Gülen na wafuasi wake waliopandikizwa katika taasisi za mahakama, jeshini, taasisi za kielimu na kwenye asasi nyingine za serikali, ndio waliopanga na kuendesha jaribio hilo.

Hivi sasa Fethullah Gülen anaishi nchini Marekani, na serikali ya nchi hiyo inakataa kumkabidhi kwa serikali ya Uturuki.