Sisitizo la Trump la kuendelea kuwepo askari wa Marekani nchini Afghanistan
(last modified Sat, 31 Aug 2019 06:38:38 GMT )
Aug 31, 2019 06:38 UTC
  • Sisitizo la Trump la kuendelea kuwepo askari wa Marekani nchini Afghanistan

Miaka 18 iliyopita Marekani iliishambulia na kuivamia kijeshi Afghanistan na kisha ikaikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kisingizio cha kulipiza kisasi cha mashambulio ya Septemba 11, mwaka 2001 na pia kupambana na ugaidi nchini humo. Wakati rais wa sasa wa Marekani Donald Trump alipokuwa kwenye kampeni za uchaguzi wa urais mwaka 2016 na baada ya kuingia Ikulu ya White House aliahidi kwamba atawaondoa askari wa nchi hiyo walioko Syria na Afghanistan, hata hivyo hadi sasa amehalifu ahadi yake hiyo.

Moja ya jumbe alizoandika Trump mwaka 2012 kuhusu kuondoa askari wa Marekani Afghanistan kabla hajawa rais

Katika msimamo wake mpya aliotangaza kuhusu suala hilo wakati alipohojiwa na kanali ya televisheni ya Fox News siku ya Alkhamisi ya tarehe 29 Agosti, Trump alitamka kuwa, askari wa Marekani wataendelea kubaki nchini Afghanistan kwa ajili ya masuala ya kiintelijensia hata kama Washington itafikia makubaliano na kundi la Taliban. Alipoulizwa kama askari wa Marekani walioko Afghanistan watendelea kubaki nchini humo au la baada ya makubaliano ambayo huenda Washington ikafikia na kundi la Taliban, Trump alijibu kwa kusema: "Inapasa tuendelee kuwepo huko kwa kiwango fulani; na tutafanya hivyo. Japokuwa idadi ya askari wetu huko itapungua kwa kiwango kikubwa, lakini tutaendelea kuwepo huko daima, na kuwepo kwenyewe kutakuwa kwa kiwango cha juu zaidi katika masuala ya kiintelijensia." 

Ujumbe mwengine alioandika Trump mwaka 2013 kuhusu uvamizi wa kijeshi wa Marekani Afghanistan

Pamoja na kutangaza kwamba idadi ya askari wa Marekani waliopelekwa Afghanistan inaendelea kupungua na imefikia askari 8,600, Trump alisema: Tutachukua uamuzi wa kupunguza askari zaidi kwa kuzingatia mabadiliko yatayojiri siku ya usoni.

Uamuzi huo uliotangazwa na Trump umekuja baada ya kikao muhimu alichofanya rais huyo wa Marekani wiki mbili nyuma na baadhi ya maafisa wa serikali yake kujadili mchakato wa kuwaondoa askari wa nchi hiyo walioko Afghanistan. Sambamba na hayo, duru ya tisa ya mazungumzo ya Marekani na kundi la Taliban ingali inaendelea nchini Qatar, ambapo hivi karibuni pia na kinyume mwenendo wa mazungumzo hayo ambayo ajenda yake kuu ni suala la kuondoka askari wa Marekani nchini Afghanistan, Trump alisisitiza kwamba hakuna haraka wala haja yoyote ya kuandaa ratiba ya kuainisha wakati wa kuwaondoa askari hao. Matamshi hayo ya Trump yamezidi kutoa changamoto ya mvutano kwa wawakilishi wa Taliban na Marekani wanaoshiriki kwenye mazungumzo ya Qatar.

Maafisa waandamizi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon wamechukua msimamo na muelekeo unaofanana na wa Trump wa kutilia mkazo kuendelea kuwepo kijeshi nchi hiyo Afghanistan. Jenerali Joseph Dunford, Mkuu wa vikosi vya majeshi ya Marekani, alitangaza siku ya Jumatano ya tarehe 28 Agosti kuwa, madamu machafuko hayajapungua nchini Afghanistan na vikosi vya Kiafghani havijawa na uwezo wa kudhibiti hali ya mambo, Washington haitaanza kutekeleza mchakato wa kupunguza askari wake.  

Jenerali Joseph Dunford

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri wake wa ulinzi Mark Esper, afisa huyo mwandamizi wa jeshi la Marekani alisema, ni mapema mno kuripoti kuwa karibuni hivi Marekani itachukua hatua ya angalau kupunguza idadi ya askari wake walioko Afghanistan. Si hayo tu, Mkuu huyo wa majeshi ya Marekani hakukanusha pia taarifa ya kuendelea kuwepo idadi kadhaa ya askari wa nchi hiyo nchini Afghanistan kwa ajili ya eti kupambana na ugaidi, hata kama Washington itafikia makubaliano na kundi la Taliban. Jenerali Dunford, ambaye ameshawahi kuongoza vikosi vya majeshi ya kigeni nchini Afghanistana amedai pia kwamba, katika mazingira ya usalama yaliyopo hivi sasa, vikosi vya Afghanistan vingali vinahitaji msaada wa askari wa Marekani.

Baadhi ya wanajeshi wa Marekani walioko Afghanistan

Misimamo inayogongana ya Trump kuhusu kuondoka kwa askari wa Marekani nchini Afghanistan na msimamo wake mpya wa karibuni kwamba askari hao wataendelea kuwepo nchini humo, kwanza vinaashiria utata na kutoeleweka wazi malengo na hatua za nje ya nchi zinazochukuliwa na serikali ya Marekani; na wakati huohuo zinadhihirisha tofauti za ndani zilizopo kati ya rais wa Marekani na mfumo wa utawala wa nchi hiyo juu ya kuwepo kijeshi Washington nchini Afghanistan. Hivi sasa askari wa Marekani wangaliko nchini Afghanistan; na hiyo ni ishara kwamba, mfumo wa utawala umeyapiku maamuzi ya Ikulu ya White House huku ikiwa haijulikani kuwepo kwa askari hao kutaendelea kwa muda gani. Na hii ni pamoja na kuwa, ili kuweza kushinda uchaguzi wa urais utakaofanyika Novemba 2020, Trump anahitaji kupata mafanikio kadhaa katika uga wa siasa za nje; na hapana shaka kwamba moja ya mafanikio hayo ni kuviondoa vikosi vya jeshi la Marekani katika ardhi ya Afghanistan.../