Shambulizi la 'drone' ya Marekani laua wakulima 30 Afghanistan
Ndege isiyo rubani ya Marekani imetekeleza shambulizi la anga na kuua makumi ya wakulima nchini Afghanistan.
Maafisa wa serikali ya Kabul wameliambia shirika la habari la Reuters Alkhamisi kuwa, drone hiyo ya Marekani ilitekeleza hujuma hiyo dhidi ya mkusanyiko wa wakulima katika mji wa Wazir Tangi, mashariki wa mkoa wa Nangarhar, ambapo 30 miongoni mwao wameuawa.
Aidha Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imethibitisha habari ya kutokea kwa shambulizi hilo la drone ya Marekani, ingawaje haijatoa takwimu ya wahanga wa hujuma hiyo.
Mkuu wa baraza la wazee wa kikabila katika eneo hilo, Malik Rahat Gul amenukuliwa na shirika la Reuters akisema kuwa, "Wakulima hao walikuwa wanaota moto nyakati za jioni baada ya kumaliza shughuli zao za ukulima mchana kutwa, wakati walipouawa katika shambulizi la drone."
Ukosefu wa amani umeongezeka nchini Afghanistan katika hali ambayo, Marekani na waitifaki wake wametuma majeshi nchini humo tangu mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kudhamini amani na usalama wa nchi hiyo.
Viiongozi wa Kabul wanasisitiza kuwa, uwepo wa vikosi vya kigeni nchini Afghanistan haujasaidia chochote ghairi ya kuongeza machafuko, ugaidi na uzalishaji wa madawa ya kulevya.