Kimbunga Hagibis chaua watu 36 nchini Japan
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na kimbunga Hagibis mashariki na katikati mwa Japan imeongezeka na kufikia 36.
Shirika la habari la Kyodo limesema mbali na makumi ya watu kuaga dunia, wengine 17 hawajulikani waliko kufikia sasa. Athari za dhoruba la Hagibis zimeonekana zaidi katika mikoa sita ya mashariki na katikati mwa Japan.
Tufani hiyo imepelekea asilimia kubwa ya miji na nyumba laki tano zibaki bila umeme huku mfumo wa mawasiliano ukikatika.
Treni na safari za ndege za karibu na mji mkuu Tokyo zilikuwa zimesimamishwa kutokana na athari za kimbunga hicho, lakini zinatazamiwa kuanza kazi tena leo Jumatatu.
Kutokana na kimbunga hicho kusafiri kwa kasi ya kilomita 180 kwa saa, maporomoko ya ardhi yametokea katika maeneo kadhaa ya nchi. Vyombo vya dola vinafanya jitihada za kuwahamisha watu zaidi ya milioni sita katika Kisiwa cha Honshu na kupelekwa nyanda za juu.
Kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa la Japan, kimbunga hicho kinaweza kuwa kikali zaidi kuwahi kutokea nchini humo ndani ya miaka 60 iliyopita.