Trump na misimamo ya undumakuwili kuhusu magaidi wa Daesh (ISIS)
Licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kutoa onyo kuhusiana na kuibukka upya shughuli za kundi la kigaidi la Daesh (ISIS), kitendo cha kuondoa askari wa Kimarekani katika maeneo yanayoshambuliwa na Uturuki huko kaskazini mwa Syria, kimeandaa uwanja wa kufufuka upya kundi hilo la ukufurishaji ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Aidha licha ya wanamgambo wa Kikurdi huko kaskazini mwa Syria kutahadharisha kuhusiana na kutoroka wafungwa wa Daesh kutoka katika jela na kambi za eneo hilo, lakini hujuma za Uturuki zimewaandalia magaidi hao wa ISIS uwezekano huo. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, kwa akali magaidi 800 wa Daesh (ISIS) wametoroka kutoka katika kambi zinazodhibitiwa na Wakurdi wa Syria, kaskazini mwa nchi hiyo. Licha ya ukweli huo, hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani ameitaka Uturuki na Wakurdi wa Syria kuzuia kutoroka magaidi wa Daesh kaskazini mwa nchi hiyo. Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter Trump ameandika: "Tunao magaidi wabaya zaidi wa Daesh. Uturuki na Wakurdi hawapasi kuwaruhusu magaidi wa Daesh kukimbia. Ulaya ni lazima iwapokee magaidi hawa na suala hilo linatakiwa kufanyika hivi sasa. Kamwe hatutoruhusu watu hao waingie ardhi ya Marekani." Uturuki ilianzisha operesheni ilizozipa jina la 'Chemchem ya Amani' wiki iliyopita huko kaskazini mwa Syria kwa lengo la kile inachokiita kuwa ni 'kulinda mipaka ya Uturuki na kuisafisha kutokana na magaidi na pia kudhamini usalama wa kurejea wakimbizi.' Hivi sasa mashambulizi ya jeshi la Uturuki dhidi ya jela na kambi za magaidi wa Daesh, yameandaa mazingira ya kutoroka magaidi hao pamoja na familia zao. Kwa sasa kuna karibu wafungwa wa Daesh elfu 11 kaskazini mwa Syria. Kuhusiana na suala hilo gazeti la Kimarekani la New York Times limewanukuu maafisa wawili wa serikali ya Washington wakisema: "Baada ya kuanza mashambulizi ya Uturuki kaskazini mwa Syria, Jeshi la Marekani limewaachilia huru makumi ya viongozi wa Daesh waliokuwa wanashikiwa, hasa baada ya askari hao kutoka katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo."
Ripoti ya gazeti hilo imetolewa baada ya kuenea taarifa zinazosema kuwa, mamia ya wanachama wa kundi la Daesh (ISIS) wamekimbia kutoka katika kambi za wapiganaji wa Kikurdi mahala walipokuwa wanashikiliwa baada ya Uturuki kuanzisha mashambulizi yake kaskazini mwa Syria, na baada ya kambi hizo kukosa usalama. Kwa utaratibu huo, ni wazi kwamba kitendo cha Marekani kufanya makusudi ya kuwaachilia huru wanachama hao wa Daesh nchini Syria, kina lengo la kulifufua upya kundi hilo la ukufurishaji ambapo inatazamiwa kuwa baada ya kukamilisha mipango yake kundi hilo litaanzisha tena operesheni zake za jinai ndani ya taifa hilo la Kiarabu. Ukweli ni kwamba Trump ni mwenye undumakuwili katika uwanja huo. Hii ni kwa kuwa kwa upande mmoja anadai kuwa kundi la Daesh nchini Syria limeangamizwa kikamilifu na kwa msingi huo haoni sababu ya kuendelea kubakia askari wa Kimarekani nchini humo, na kwa upande mwingine ameitahadharisha Uturuki na Wakurdi kuwa makini na magaidi wa Daesh na kuwataka wasiwaruhusu watenda jinai hao watoroke. Swali muhimu la kujiuliza ni hili kwamba, je, baada ya Uturuki kuanzisha mashambulizi makali ya anga na ardhini nchini Syria, ni vipi Trump anawataka Wakurdi waendelee kuwazuilia wanachama wa Daesh, tena katika hali ambayo mashambulizi hayo yameandaa fursa nzuri kwa magaidi hao kukimbia na kisha kuratibu upya shughuli zao? Kuhusiana na suala hilo, James N. Mattis Waziri wa Ulinzi wa zamani wa Marekani amesema kuwa: "Iwapo Washington haitaendeleza mashinikizo yake dhidi ya Daesh nchini Syria, basi kundi hilo la kigaidi litafufua na kuhuisha tena shughuli zake."
Kwa upande mwingine ni kwamba Trump ameubebesha Umoja wa Ulaya dhima ya magaidi wa Daesh wanaoshikiliwa kaskazini mwa Syria, na kuzitaka nchi za umoja huo ziwapokee magaidi hao. Kidhahiri rais huyo wa Marekani amesahau kuwa muhusika mkuu wa kuundwa na kustawishwa kundi hilo hatari la kigaidi ni serikali yenyewe ya Washington. Hata katika kampeni zake za uraisi zilizomuingiza madarakani mwaka 2016, Trump alisikika mara nyingi akisema kuwa, serikali ya Barack Obama ndiyo iliyoanzisha kundi la Daesh (ISIS). Katika moja ya mikutano hiyo ya kampeni Trump alisema: "Obama na Hillary Clinton ni watu wasio wakweli. Wao ndio waliunda kundi la Daesh. Hillary Clinton kwa kushirikiana na Barack Obama ndio walioanzisha kundi hilo." Inafaa kuashiria kuwa, baada ya Marekani kulitumia kundi hilo la ukufurishaji kama wenzo wa kufikia malengo yake, sasa inakusudia kuziwekea mashinikizo nchi za Ulaya kwa kuwasukuma magaidi hao katika nchi hizo. Hata hivyo nchi hizo hazipo tayari kuwapokea magaidi hao hatari. Ukweli ni kwamba hatua ya Trump kuiruhusu Uturuki kushambulia kaskazini mwa Syria, ambayo natija yake ni kutoroka magaidi hao na hatimaye kuratibu upya shughuli zao, inakusudia kuandaa uwanja wa kuwekewa mashinikizo zaidi serikali ya Syria, kuibua ghasia ndani ya nchi hiyo na Iraq na pia kuzitwisha nchi za Ulaya tatizo la wanachama wa Daesh (ISIS), suala ambalo kiujumla ni kukimbia Washington majukumu yake.