Waislamu Ujerumani wazidi kuandamwa na vitendo vya chuki na ubaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57017-waislamu_ujerumani_wazidi_kuandamwa_na_vitendo_vya_chuki_na_ubaguzi
Mmoja wa viongozi wa Kiislamu nchini Ujerumani amesema kuwa, Waislamu wa nchi hiyo ya bara Ulaya wanazidi kuandamwa na mashambulio ambayo chimbuko lake ni vitendo vya ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 03, 2019 02:32 UTC
  • Waislamu Ujerumani wazidi kuandamwa na vitendo vya chuki na ubaguzi

Mmoja wa viongozi wa Kiislamu nchini Ujerumani amesema kuwa, Waislamu wa nchi hiyo ya bara Ulaya wanazidi kuandamwa na mashambulio ambayo chimbuko lake ni vitendo vya ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Burhan Kesici, Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani anasema kuwa, katika mwaka huu kumeshuhudiwa zaidi ya mashambulio 80 dhidi ya misikiti nchini humo hali ambayo inaonyesha ni kwa kiasi gani hali ya amani kwa Waislamu ni mbaya katika nchi hiyo.

Kiongozi huyo wa Kiislamu anasema kuwa, maafisa usalama wa Ujerumani wanahitaji kuwa na ushirikiano wa karibu na jamii ya Kiislamu, kuongeza ufahamu, welewa pamoja na ushauri kuhusiana na Uislamu na Waislamu.

Kadhalika amesema kuwa, kuongezeka vitendo vya mashambulio dhidi ya misikiti kumewafanya Waislamu wa nchi hiyo ya Ulaya waishi katika hali ya wasiwasi na hofu kubwa kutokana na kuhisii kwamba, hawana amani.

Maandamano ya kulalamikia chuki dhidi ya Uislamu

Takwimu zinaonyesha kuwa, katika mwaka uliopita wa 2018, zaidi ya misikiti na taasisi 100 za Kiislamu nchini Ujerumani zilishambuliwa na makundi ya kufurutu ada ya mrengo wa kulia yenye chuki na Uislamu na Waislamu.

Aidha katika mwaka uliopita, polisi ya Ujerumani ilisajili makosa na vitendo vya uhalifuu 813 dhidi ya Waislamu yakiwemo ya matusi, barua za vitisho na hata mashambulio ya kupigwa ambayo yalipelekea kujeruhiwa kwa akali Waislamu 54.

Ujerumani yenye wakazi takribani milioni 84 ni nchi ya pili yenye Waislamu wengi barani Ulaya baada ya Ufaransa.