Mkutano wa BRICS na tahadhari ya Putin kuhusu vikwazo vya Marekani
Viongozi wa nchi wanachama katika jumuiya ya BRICS unayojumuisha nchi tano za Russia, Brazil, China, India na Afrika Kusini wamekutana katika mji mkuu wa Brazil, Brasilia. Mkutano huo umefanyika katika siku za tarehe 13 na 14 na ulilenga kupanua zaidi ushirikiano wa masuala ya kifedha na kiuchuni baina ya nchi wanachama na kuleta mabadiliko katika muundo wa sasa wa kimataifa.
Mkutano wa kwanza wa viongozi wa nchi za BRICS ulifanyika nchini Russia mwaka 2009. Nchi wanachama wa kundi hili ni wajumbe muhimu sana katika kundi la G20 na zinafanya mikakati ya kuzidisha ushawishi na taathira ya kundi hilo katika masuala ya uchumi wa kimataifa. Inatabiriwa kuwa, uchumi wa nchi wanachama wa BRICS utapiku na kuzidi ule wa nchi zilizoendelea kiviwanda maarufu kama G7, na jambo hilo linaonesha zaidi umuhimu wa BRICS katika uwanja wa uchumi, biashara na siasa za kimataifa. Kwa msingi huo Marekani inapinga vikali kuimarika na kupata nguvu kundi hili na inafanya kila iwezalo kulinda nafasi yake katika medani ya kimataifa kupitia njia ya kutumia mabavu na kuzitwisha nchi nyingine matakwa yake.
Mwenendo huo wa Marekani ambao umeshika kasi zaidi katika kipindi cha utawala wa Donald Trump ikiwa ni pamoja na vita vya kibiashara vya nchi hiyo dhidi ya China, umekosolewa vikali na Russia ambayo ni mwanachama muhimu katika jumuiya ya BRICS. Rais Vladimir Putin amesema katika hotuba yake kwenye mkutano wa viongozi wa BRICS mjini Brasilia kwamba: "Hivi sasa ushindani usio wa kiadilifu unaonekana zaidi katika medani ya biashara ya kimataifa kuliko wakati wowote mwingine. Hapana shaka kuwa katika mazingira ya sasa uchumi wa dunia umeathiriwa sana na mbinu za ushindani zisizo za kiadilifu ikiwa ni pamoja na vikwazo vya upande mmoja vinavyochochewa na malengo na matashi ya kisiasa. Suala hili linazuia ustawi wa kiuchumi wa nchi mbalimbali."
Matamshi haya ya Putin yamelenga siasa na misimamo ya Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ametangaza waziwazi kwamba nchi hiyo inapaswa kuwa juu ya nchi nyingine, na ulazima wa nchi za dunia kufuata siasa na sera za serikali ya Washington. Trump pia anatekeleza siasa za kuzidisha ushuru wa forodha kwa bidhaa za nchi nyingine zinazoingizwa Marekani, kuweka vizuizi mbalimbali kwa kutumia visingizio vya kulinda bidhaa za ndani na vilevile kuweka vikwazo vya upande mmoja kwa shabaha ya kuwafutilia mbali wapinzani wa kibiashara wa Washington. Katika uwanja huu Waziri Mkuu wa Russia Dmitry Medvedev mapema mwezi huu wa Novemba alitahadharisha kwamba: "Siasa za vikwazo za Marekani zitazusha vita kubwa ya kibiashara."
Kwa kutilia maanani hali hiyo, nchi wanachama wa BRICS zimechukua matua maalumu za kustawisha uchumi wao na kuzuia jambo lolote linaloweza kuhatarisha hali bora ya raia wa nchi hizo. Wanachama wa BRICS wamekosoa vikali siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani na wametoa wito wa kuwepo mfumo wa kambi kadhaa za kibiashara ni kulinda biashara ya kimataifa, kuzuia ubaguzi katika uwanja huo na kudhamini uhuru wa sekta hiyo. Vilevile wanachama wa jumuiya hiyo wametaka kuwepo mapambano dhidi ya hatua za kibaguzi za kibiashara hususan sera za kibiashara za Donald Trump.
Katika uwanja huo Rais Vladimir Putin wa Russia ametangaza kuwa, Moscow inakusudia kuwasilisha mpango kabambe na maalumu wa kiuchumi kwa ajili ya ustawi na ushirikiano baina ya nchi za kundi la BRICS katika mkutano ujao wa nchi wanachama uliopangwa kufanyika Julai mwaka 2020 katika mji wa Saint Petersburg nchini Russia.