Baraza la Usalama lazionya nchi zinazoendelea kumimina silaha Libya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57647-baraza_la_usalama_lazionya_nchi_zinazoendelea_kumimina_silaha_libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa onyo kali kwa nchi zinazokiuka azimio la baraza hilo na kuendelea kurundika silaha nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 03, 2019 07:35 UTC
  • Baraza la Usalama lazionya nchi zinazoendelea kumimina silaha Libya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa onyo kali kwa nchi zinazokiuka azimio la baraza hilo na kuendelea kurundika silaha nchini Libya.

Hivi karibuni, wachunguzi wa UN walizituhumu Imarati, Jordan na Uturuki kuwa zimekiuka vikwazo hivyo vya Baraza la Usalama, kwa kuendelea kutuma silaha nchini Libya.

Kadhalika Baraza la Usalama la UN limezitaka nchi za dunia kujiepusha na uingiliaji wa masuala ya ndani ya Libya. Taarifa hiyo iliyosainiwa jana Jumatatu na nchi 15 wanachama wa baraza hilo inasema, "Tunazitaka nchi zote ziheshimu vikwazo vya silaha dhidi ya Libya, na zijiepushe na hatua ambazo zinaweza kushadidisha mgogoro wa nchi hiyo."

Indhari hiyo ya Baraza la Usalama imetolewa katika hali ambayo, usiku wa kuamkia jana, vikosi vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya vinavyoongozwa na Khalifa Haftar viliripotiwa kufanya mashambulizi ya anga katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli ambayo yaliua watoto watano. 

Makombora ya US yaliyonaswa Libya na jeshi la Serikali ya Muafaka wa Kitaifa

Huku hayo yakijiri, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umelaani vikali mauaji ya watoto katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na wapiganaji wa Haftar viungani mwa Tripoli na katika mji wa Umm al-Aranib, yapata kilomita  765 kutoka Tripoli.

Serikali ya Muafaka wa Kitaifa yenye makao makuu yake mjini Tripoli na inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa imesema watoto 14 na wanawake wawili ni miongoni mwa watu waliouawa katika mashambulizi hayo mapya ya wanamgambo wa Haftar, tokeo Ijumaa.