Dec 06, 2019 08:04 UTC
  • Sera za undumilakuwili za Marekani nchini Syria

Tangu mwaka 2014, Marekani imejiingiza kijeshi kinyume cha sheria nchini Syria kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Daesh; na hivi sasa pia, licha ya madai ya rais wa nchi hiyo Donald Trump kwamba imejiondoa kijeshi katika ardhi ya Syria, imeshatafuta kisingizio kingine kipya ili kurefusha muda wa kuweko askari wake nchini humo.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper, ametangaza kukamilika mchakato wa kuondoka kundi moja la skari wa nchi hiyo katika eneo la kaskazini mwa Syria na kusisitiza kwamba, idadi nyingine ya wanajeshi wa Marekani itaendelea kubakia katika maeneo mengine ya ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa mujibu wa Esper, sambamba na kutangazwa kukamilika mchakato wa kuondoka askari wa Marekani nchini Syria, baada ya hatua hiyo, wanajeshi wengine wapatao 600 watawekwa katika maeneo mengine ya Syria; na endapo itahitajika, kuna uwezekano wa kuongezwa idadi ya askari hao. 

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mark Esper

Wakati alipokuwa akirejea Marekani kutoka London alikokwenda kuhudhuria mkutano wa shirika la kijeshi la NATO, mkuu huyo wa Pentagon alitangaza Jumatano usiku: "Idadi hii itakuwa takribani ya kudumu, lakini endapo yatajiri matukio yasiyotabirika ... tunaweza kufanya mabadiliko." Waziri wa Ulinzi wa Marekani amedai kwamba, ikiwa washirika wa Washington watashiriki katika operesheni za Syria, yumkini idadi ya askari wa Marekani walioko nchini humo ikapunguzwa. Esper ameongeza kuwa: Ikiwa nchi moja muitifaki, nchi moja mwanachama wa NATO itaamua kutupatia askari 50, tunaweza kuwarudisha nyumbani askari 50.

Mnamo mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba, Rais Donald Trump wa Marekani aliamuru askari wa nchi hiyo waondoke nchini Syria. Kuanzia wakati huo, idadi ya wanajeshi wapatao elfu moja wa Marekani waliokuweko nchini humo, imepungua kwa karibu asilimia 40. Japokuwa tangu mwaka uliopita hadi sasa, rais wa Marekani amekuwa akisisitiza kila mara kuhusu kuondoka askari wa nchi hiyo katika ardhi ya Syria, lakini wakati huohuo amekuwa akieleza pia kwamba, baadhi ya askari hao wangaliko katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, hususan ya visima vya mafuta; suala ambalo linakinzana waziwazi na sera inayopigiwa upatu na Ikulu ya White House ya kuondoka kikamilifu katika ardhi ya Syria.

Baadhi ya wanajeshi wa Marekani wakionekana kuondoka katika ardhi ya Syria

Marekani imepiga kambi kijeshi nchini Syria tangu mwaka 2014 hadi sasa kupitia kile ilichokipa jina la muungano wa kupambana na Daesh. Uwepo huo wa kijeshi wa Marekani ni haramu na unafanyika kinyume cha sheria, kiasi kwamba umekuwa ukilaaniwa vikali na serikali halali ya Syria na vile vile Russia, ambayo ni muitifaki mkuu wa serikali ya Damascus. Mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Novemba, rais wa Marekani, na licha ya ahadi aliyotoa ya askari wa nchi hiyo kuondoka nchini Syria, alitamka kuwa baadhi ya askari hao watendelea kubakia kwenye maeneo ya visima vya mafuta vya nchi hiyo mashariki mwa Mto Euphrates; ambako ndiko iliko asilimia 90 ya nishati ya mafuta ya Syria. Lindsey Graham, seneta wa Marekani mwenye misimamo ya kufurutu mpaka aliwahi kupendekeza kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba gharama za kuwahudumia askari wa nchi hiyo walioko Syria zifidiwe kupitia mauzo ya mafuta ya nchi hiyo. 

Alipozungumza na waandishi wa habari mjini London pembeni ya kikao cha NATO, Rais Donald Trump wa Marekani alisema: "Daesh inafanya juu chini ili kuvidhibiti vyanzo vya mafuta ya Syria, lakini kwa sasa, sisi tumedhibiti vyanzo hivyo kikamilifu...Kati ya askari wetu walioko kwenye maeneo ya ardhi ya Syria, ni wale wanaolinda visima vya mafuta tu ndio waliobakia. Mafuta ya Syria yako mikononi mwetu na tunaweza kuyafanya vyovyote tutakavyo.

Rais Bashar al-Assad wa Syria (kushoto) na Rais Vladimir Putin wa Russia

Serikali ya Syria imekuwa ikisisitiza kila mara kuwa kuwepo kijeshi Marekani nchini humo kumefanyika bila kibali cha serikali hiyo; na kuendelea Washington kulikalia kwa mabavu eneo la mashariki ya Syria kunafanyika kwa lengo la kupora maliasili za nchi hiyo na hasa mafuta. Bashar al-Jaafari, balozi na mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa Marekani imevamia na kuvikalia kwa mabavu visima mafuta vya Syria na inapora na kuiba mali za nchi hiyo huku ikinyamaziwa kimya na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kinyume na madai ya kila mara ya Trump kuhusu kuondoka askari wa Marekani katika ardhi ya Syria, vyombo vya utawala vya Washington havikubaliani hata kidogo na mtazamo wake huo; na ndiyo maana mashinikizo ya bunge la nchi hiyo yamemfanya Trump aridhie kubakisha askari wapatao 600 katika eneo la mashariki ya Syria kwa kisingizio cha eti kulinda visima vya mafuta vya eneo hilo visije vikavamiwa na kuhujumiwa na Daesh.

Marekani imedhamiria kuyapora na kuyatumia mafuta ya Syria ilhali kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ni haramu na kinyume cha sheria kutumia maliasili za nchi yoyote huru na inayojitawala bila kibali cha serikali ya nchi hiyo.../

Tags