Vitisho vya Trump vya kuiwekea vikwazo Iraq, kushindwa kwingine kwa Washington
Jinai kubwa ya Marekani ya kumuua kigaidi Meja Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi Al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq, imeibua radiamali kali ya bunge la nchi hiyo ya Kiarabu na kuipelekea kupitisha sheria ya kuvitimua vikosi vya muungano vamizi wa eti kupambana na Daesh (ISIS) unaojumuisha askari wa Marekani.
Suala hilo limemfanya Rais Donald Trump wa Marekani kutoa radiamali yake iliyosukumwa na wahka mkubwa. Kufuatia kupasishwa sheria hiyo inayowataka askari wa Marekani kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo, Trump ameitisha Baghdad kwamba itakumbwa na vikwazo vikali vya Washington. Trump amesema: "Tutaondoa askari wetu Iraq, lakini Wairaki watatakiwa walipe gharama za ujenzi wa kambi ya jeshi la anga ya Marekani nchini humo." Tarehe tano mwezi huu wabunge wa Iraq na katika hatua ya kuhitimisha uwepo wa askari vamizi wa kigeni nchini kwao, walipasisha sheria ambayo inawataka askari hao kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo. Adil Abdul-Mahdi, Waziri Mkuu wa Iraq alilitaka bunge hilo kupiga kura ya kupitisha mpango wa kuwatimua haraka askari hao wa kigeni kutoka ardhi ya Iraq kwa kusema: "Maslahi ya Iraq na Marekani yatakuwa katika amani wakati askari wa kigeni wataondoka Iraq." Hatua hiyo ambayo haikutarajiwa, imewafanya Wamarekani kupatwa na wahka na hivyo kujipata wakitoa radiamali ya pupa na yenye utata kwa kuwataka Wairaki waangalie upya sheria hiyo. Wamarekani wamedai kwamba maslahi ya Iraq yanategemea kudumishwa uhusiano na Washington. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imedai kwamba kupasishwa mpango wa kuwafurusha askari wa kigeni kutoka ardhi ya Iraq, kumeivunja sana moyo Washington. Morgan Ortagus, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema: "Sisi tunawataka viongozi wa Iraq kuangalia upya umuhimu wa uhusiano wa kiuchumi na kiusalama wa nchi mbili na umuhimu wa uwepo wa muungano wa kuliangamiza kundi la Daesh (ISIS)." Serikali ya Trump ilijaribu kila ililoweza kuwashawishi viongozi wa Iraq wazuie sheria hiyo iliyopitishwa na bunge kuhusiana na kutimuliwa askari wa kigeni kutoka nchi hiyo, hata hivyo lobi za Washington zilishindwa kufikia lengo hilo. Inaonekana kuwa, katika hali ambayo Marekani yenyewe ilikuwa ikitaraji kwamba baada ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC na Abu Mahdi Al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq ya Hashdu sh-Sha'abi, ingeweza kuimarisha udhibiti wake kikamilifu juu ya Iraq, lakini sasa ni yenyewe ndio inalazimishwa kuondoka katika nchi hiyo.

Kadhalika serikali ya Trump ilikuwa ikidhani kwamba kwa jinai yake hiyo ya kinyama, ingeweza kuondoa vizuizi vinavyoizuia kuidhibiti kikamilifu Iraq ambapo katika hatua ya pili ilikuwa imejiandaa kuimaliza kabisa Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi. Aidha rais huyo wa Marekani alidhani kuwa, kwa hatua yake ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani si tu kwamba ingefanikiwa kuiogopesha Iran, bali ingekuwa imeutumikia kwa kiwango kikubwa utawala haramu wa Israel sambamba na kutoa pigo kubwa kwa mrengo wa muqawama. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si tu kwamba imetishia kulipiza kisasi kikali kwa Marekani, bali serikali na bunge la Iraq pia zimebeba bendera ya kutaka kuondolewa askari wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo. Kwa mara kadhaa katika kampeni zake za uchaguzi na baada ya hapo, Trump alitoa kauli kwamba angewaondoa askari wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, hata hivyo kivitendo katika miezi ya hivi karibuni amechukua hatua kinyume ya kutuma askari zaidi katika eneo hili. Kiasi kwamba kwa akali askari elfu 14 wa Kimarekani wametumwa katika eneo hususan Ghuba ya Uajemi. Wakati huo huo Trump hivi sasa anakabiliwa na matatizo mengi, yaani hatua ya ulipizaji kisasi wa Iran kwa damu ya Meja Jenerali Qassem Soleimani. Baada ya kumuua kigaidi Luteni Qassem Soleimani, Trump aliitaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulipuuza suala hilo na kuliona kuwa lililopita kirahisi tu. Jibu la moja kwa moja la Tehran kwa takwa hilo la Washington la kutolipizwa kisasi kikali kwa Marekani, limemtia kiwewe Trump.

Na kutokana na kufeli juhudi zake za kujaribu kupunguza hasira za Wairani, na hatimaye aweze kukimbia dhima ya kisasi kutoka kwa Iran na muqawama, ndio maana akatoa vitisho visivyo vya kipumbavu kwa lengo la kuitisha Tehran. Katika uwanja huo, Jumapili iliyopita na kwa mara nyingine aliitishia kijeshi Iran na kudai kwamba iwapo Tehran itayalenga maslahi yake au Wamarekani, basi itapata jibu kali kutoka kwa Washington. Pamoja na hayo kwa kipindi cha miaka 40 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha kwamba kamwe haitishiki na vitisho vya Washington na daima imekuwa ikitoa jibu kali kwa shari za Marekani katika eneo. Hivi sasa Washington si tu kwamba inatakiwa isubirie jibu kali la kisasi kutoka kwa Iran, bali sasa inatakiwa kufunga virago vyake na kuondoka Iraq, suala ambalo linahesabika kuwa ni kushindwa kwingine kwa siasa za kigeni za Trump katika mwaka wake huu anaogombea uchaguzi wa rais wa Marekani.