Wajapani waandamana kupinga ubeberu wa Marekani
Raia wa Japan wamefanya maandamano makubwa mjini Tokyo kupinga siasa za kutaka vita za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Waandamanaji walipiga kambi mbele ya ofisi ya Waziri Mkuu wa Japan, Shinzō Abe na ubalozi wa Marekani mjini Tokyo huku wakipiga nara za kulaani vita na kuilaani Marekani. Kadhalika waandamanaji wameitaka serikali ya nchi hiyo kusitisha mpango wa kutuma askari kwenda eneo la Asia Magharibi. Hii ni katika hali ambayo vyombo vya habari nchini humo viliakisi shambulio la makombora la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye ngome za jeshi la Marekani nchini Iraq, na kubainisha kuwa Tehran imetoa jibu kufuatia jinai ya kigaidi ya kumuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani. Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC, Ijumaa Alfajiri 3 Januari aliwasili nchini Iraq kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa nchi hiyo.

Punde baada ya kuwasili, akiwa ndani ya gari pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq maarufu kama al Hashdu sh-Sha'abi pamoja na watu wengine wanane, walishambuliwa tokea angani na wanajeshi vamizi na wa kigaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad na wote wakauawa shahidi katika tukio hilo. Kufuatia unyama huo Jumatano usiku Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran lilivurumisha makumi ya makombora na kuzipiga kambi za jeshi la Marekani mkoani Al-Anbar na Erbil nchini Iraq.