Radiamali za nchi zilizowekewa vikwazo vya usafiri na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58895-radiamali_za_nchi_zilizowekewa_vikwazo_vya_usafiri_na_marekani
Serikali ya Eritrea imekosoa vikali hatua ya Washington ya kuwawekea vizingiti raia wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wanaotaka kwenda Marekani ikisisitiza kuwa, vikwazo hivyo vya usafiri havikubaliki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 02, 2020 04:04 UTC
  • Radiamali za nchi zilizowekewa vikwazo vya usafiri na Marekani

Serikali ya Eritrea imekosoa vikali hatua ya Washington ya kuwawekea vizingiti raia wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wanaotaka kwenda Marekani ikisisitiza kuwa, vikwazo hivyo vya usafiri havikubaliki.

Osman Saleh Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea ameuataja uamuzi huo wa Marekani kama hatua ya kisiasa ambayo itakuwa na athari hasi kwa uhusiano wa Asmara na Washington.

Serikali ya Nigeria ambayo pia imejumuishwa kwenye orodha hiyo mpya ya nchi zilizowekewa vizingiti hivyo kwa kuingia Marekani imesema haikupewa taarifa za awali na Washington juu ya kadhia hiyo, na kwamba imeunda kamati ya kutathmini sababu zilizopelekea kuwekewa vikwazo hivyo.

Tanzania ambayo ni nchi nyingine ya Kiafrika iliyojumuishwa katika orodha hiyo ya kibaguzi imesema haijapewa taarifa rasmi na serikali ya Marekani kuhusiana na kadhia hiyo. Emmanuel Buhohela, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki amesema, "Hatujapokea taarifa rasmi kutoka serikali ya Marekani, hatujapokea taarifa rasmi ya kidiplomasia ambayo ndiyo njia rasmi ya mawasiliano baina ya serikali mbili."

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyepigwa marufuku kuingia Marekani

Kwa mujibu wa taarifa, wahajiri kutoka Myanmar, Eritrea, Kyrgyzstan na Nigeria watazuiwa kuingia Marekani kwa viza za uhamiaji. Raia wa Sudan na Tanzania nao hawataruhusiwa kushiriki katika ule mchakato wa bahati nasibu maarufu kama green card lottery ambapo wanaofanikiwa hupata uraia wa Marekani.

Nchi hizo mpya zinaingia katika kundi la nchi nyingine saba ambazo aghalabu ya raia wake ni Waislamu, ambao wamepigwa marufuku kuingia Marekani toka mwaka 2017. 

Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi amekosoa vikali uamuzi huo wa utawala wa Trump dhidi ya uhajiri na kuutaja kama ubaguzi uliovishwa vazi la sera.