Pakistan haina imani na upatanishi wa Marekani katika mzozo wa Kashmir
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58994-pakistan_haina_imani_na_upatanishi_wa_marekani_katika_mzozo_wa_kashmir
Waziri Kiongozi wa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan amesema kuwa upatanishi wa Marekani katika utatuzi wa mzozo wa eneo hilo hautakuwa na maslahi kwa Waislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2020 02:41 UTC
  • Pakistan haina imani na upatanishi wa Marekani katika mzozo wa Kashmir

Waziri Kiongozi wa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan amesema kuwa upatanishi wa Marekani katika utatuzi wa mzozo wa eneo hilo hautakuwa na maslahi kwa Waislamu.

Akizungumza kwa mnasaba wa kushikamana na watu wa Kashmir inayodhibitiwa na India, Farooq Haider Khan amesema kuwa kuingia Marekani katika suala la Kashmir ni hatari kubwa. Waziri Kiongozi huyo ameongeza kwamba Marekani kamwe haiwezi kuingia katika mzozo huo kwa maslahi ya Wakashmir wala Waislamu na kuwa uamuzi wowote itakaouchukua kuhusiana na eneo hilo bila shaka utakuwa kwa maslahi ya Wahindi.

Matamshi ya Waziri Kiongozi huyo wa Kashmir kuhusu juhudi za Marekani za kuingilia masuala ya eneo hilo kwa kisingizio cha upatanishi yanatokana na uzoefu hasi wa nchi hiyo katika upatanishi wake wa upendeleo katika migogoro mbalimbali ya kieneo na kimataifa. Mfano wa wazi wa suala hilo ni mpango wa kidhalimu uliozinduliwa hivi karibuni na Marekani kuhusiana na mzozo wa muda mrefu zaidi katika eneo la Asia Magharibi, kwa jina la 'Muamala wa Karne' ambapo imeonyesha upendeleo wa wazi kwa utawala ghasibu wa Israel kwa madhara ya Waislamu wa Palestina.

Farooq Haider Khan

Kwa kutilia maanani kwamba serikali yenye hila na hadaa ya Marekani kupitia mpango huo wa kishetani unaoitwa 'Muamala wa Karne', imekanyaga haki zote za Waislamu na taifa dhulumiwa la Palestina huku ikiteteta kwa hali na mali maslahi haramu ya utawala ghasibu wa Israel unaoendelea kuua kikatili watoto na wanawake wa Kipalestina, rekodi ya White House katika kueneza dhulma na kukanyaga haki za Waislamu ni jambo linaloonekana wazi mbele ya walimwengu.

Ni kutokana na ukweli huo ndipo, Waziri Kiongozi wa Kshmir inayodhibitiwa na Pakistan akasema wazi kuwa uingiliaji wa Marekani katika utatuzi wa mgogoro wa Kashmir inayodhibitiwa na India bila shaka utakuwa kwa maslahi ya serikali ya New Delhi na kwa madhara ya moja kwa moja ya watu wa Kashmir.

Kwa kutilia maanani ushirikiano wa kistratijia wa Marekani na India na hasa baada ya kutiwa saini mkataba wa ushirikiano wa pande hizo katika uwanja wa nyuklia katika kipindi cha uongozi wa Barack Obama, Rais wa zamani wa Marekani, ni wazi kuwa ingiliaji wa White House katika mzozo wa Kashmir utakuwa tu kwa madhara ya watu wa eneo hilo.

Waislamu wa Kashmir wakilalamikia ukandamizaji wa serikali ya India

Licha ya kuwa ni miezi kadhaa sasa imepita tokea kupitishwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa linalotaka kuitishwa kura ya maoni katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India ili watu wa eneo hilo wapate kujiamulia wenyewe mustakbali wao wa kisiasa, lakini hakuna nchi yoyote ya Magharibi ikiwemo Marekani, ambayo imewahi kutoa mashinikizo ya kutaka kura hiyo ifanyike.

Inaonekana kuwa kanuni ya Marekani katika mizozo inayozihusisha pande za Kiislamu na zisizokuwa za Kiislamu, ni kuunga mkono na kutetea kwa nguvu zake zote upande usiokuwa wa Kiislamu kwa madhara ya Waislamu.