Polisi wa Ufaransa waimarisha mgomo wao
(last modified Sat, 08 Feb 2020 07:50:50 GMT )
Feb 08, 2020 07:50 UTC
  • Polisi wa Ufaransa waimarisha mgomo wao

Polisi wa kitengo cha 'teknolojia na elimu' nchini Ufaransa wameimarisha mgomo wao sawa na wafanyakazi wengine wa serikali katika kupinga mabadiliko ya sheria ya ustaafu nchini humo.

Mgomo wa maafisa hao wa polisi ulioanza wiki sita zilizopita katika kupinga sheria hiyo ya serikali kuhusu ustaafu, ulishuhudiwa jana mbele ya ukumbi wa Opéra Garnier mjini Paris. Washiriki wa mgomo huo ambao walikuwa wamejipaka damu bandia, walilala ardhini kwa masaa kadhaa. Polisi wa vitengo vya teknolojia na elimu nchini Ufaransa wana wajibu wa kufuatilia makosa ya jinai na kukusanya taarifa za awali, athari za vidole pamona na vijinasaba DNA kwa ajili ya uchunguzi.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Kufuatia kuendelea malalamiko na kuzorota baadhi ya sekta za Ufaransa kutokana na migomo ya kila mara iliyoanza tarehe 5 Disemba mwaka jana, serikali ya nchi hiyo imelazimika kubadili baadhi ya vipengee vya mpango wa marekebisho ya sheria ya ustaafu. Katika uwanja huo mwishoni mwa Disemba mwaka jana Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliwataka wafanya maandamano na waandaji wa migomo nchini humo kusitisha migomo hiyo na badala yake wafikie makubaliano na serikali, suala ambalo halikufikia natija.