Trump: Biden anatakiwa kujibu tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia zinazomkabili
Rais Donald Trump wa Marekani ambaye mwenyewe ana kashfa chungu nzima za kijinsia, amemtaka mshindani wake wa uchaguzi kujibu tuhuma za unyanyasi wa kijinsia zinazomkabili.
Trump amesema kuwa Joe Biden, makamu wa zamani wa rais wa nchi hiyo na ambaye pia ni mgombea wa chama cha Democrat katika uchaguzi wa 2020, ni lazima ajibu tuhuma zinazomkabili kuhusu kashfa za unyanyasaji wa kijinsia. Kadhalika rais huyo wa Marekani ambaye anakabiliwa na tuhuma chungu nzima za kuwa na mahusiano nje ya ndoa kinyume cha sheria, kashfa za kijinsia na mashtaka ya makumi ya wanawake dhidi yake, amesema kuwa hajui chochote kuhusu hilo lakini Biden anapasa kutoa majibu.
Kabla ya hapo Trump alituhumiwa na mmoja wa wacheza filamu chafu wa Marekani kwa jina la Stormy Daniels kwamba alikuwa na uhusiano haramu naye kabla ya kuwa rais, ambapo kabla ya kujiri uchaguzi mwaka 2016 rais huyo wa Marekani alimuhonga kwa ajili ya kumnyamazisha. Awali Tara Reid, mtumishi wa zamani wa ofisi ya Joe Biden aliiambia mahkama kwamba, Biden alimdhalilisha kijinsia. Kwa mujibu wa mwanamke huyo, tukio hilo lilijiri yapata miaka 30 iliyopita. Hivi sasa mgombea huyo wa chama cha Democrat katika uchaguzi wa rais wa mwaka huu anakabiliwa na mashinikizo ya ndani na nje yakimtaka ajibu tuhuma dhidi yake kuhusu unyanyasaji wa kijinsia wa mwanamke huyo. Hadi sasa Biden hajasema lolote kuhusu tuhuma hizo.