Mwanamke Mtaliano aliyesilimu akiwa Somalia atumiwa jumbe za chuki
Mwanamke mmoja raia wa Italia aliyekuwa ametekwa nyara nchini Somalia kwa karibu mwaka mmoja na nusu ameshambuliwa vikali na kutumiwa jumbe za chuki na vitisho baada ya kubainika kuwa aliukubali Uislamu akiwa mateka.
Aisha Romano ambaye kabla ya kusilimu wakati wa kutekwa kwake miezi 18 iliyopita alikuwa akifahamika kama Silvia Romano, ametumiwa jumbe za chuki na vitisho kwenye mitandao ya kijamii na watu wa matabaka mbalimbali wakiwemo wanasiasa wa Italia. Mbali na kushambuliwa vikali kwenye mitandao ya kijamii kwa kusilimu, baadhi ya magazeti ya nchi hiyo yameandika habari na makala za kumponda.
Habari kumhusu mwanamke huyo iliwekwa kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti la mrengo wa kulia la Il Giornale juzi Jumatatu, chini ya kichwa kilichojaa chuki kisemacho "Muislamu na mwenye furaha. Silvia asiye na shukurani."
Mwanasiasa mmoja katika mkoa wa Treviso, kaskazini mashariki mwa Italia alituma ujumbe kwenye ukurasa wake wa Facebook akitaka mwanamke huyo anyongwe kwa kuukubali Uislamu. Hata hivyo mtandao huo wa kijamii umefuta ujumbe huo wa chuki.
Matteo Salvini, mkuu wa chama chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia cha League nchini Italia amesema, "magaidi wa Kiislamu, wametengeza pesa, wamefanya kosa la jinai, lakini pamoja na hayo wameshinda vita vya kiutamaduni, kwa kumsilimisha na kumvisha niqabu."
Vyombo vya habari vya Italia vimeripoti kuwa, serikali ya Rome ilitoa dola milioni 1.5 na kuwapa waliomteka Romano, kama kikomboleo.
Naye Alessandro Sallusti, mkuu wa gazeti la Il Giornale linalomilikiwa na ndugu ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: "Silvia amerejea...lakini ni kana kwamba alikuwa kizuizini alikovishwa kama Mnazi. Sielewi na katu sitoelewa."
Hii ni katika hali ambayo, mwanamke huyo ambaye alikuwa akifanya kazi na shirika la kibinadamu la Africa Milele kabla ya kutekwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia ameyaambia magazeti y nchi hiyo kuwa, alisilimu mwenye pasina kushinikizwa na yoyote, baada ya kuisoma Qurani na kuujua Uislamu na kwamba hakudhalilishwa wala kuteswa na waliomteka.