Ujerumani yalaumiwa kwa kutumia vibaya mgogoro wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61045-ujerumani_yalaumiwa_kwa_kutumia_vibaya_mgogoro_wa_libya
Duru mbalimbali duniani zinailaumu Ujerumani kwa kuchochea mapigano nchini Libya na kutojali vikwazo na marufuku ya kutopeleka silaha katika nchi hiyo iliyoathiriwa vibaya na vita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 17, 2020 20:11 UTC
  • Ujerumani yalaumiwa kwa kutumia vibaya mgogoro wa Libya

Duru mbalimbali duniani zinailaumu Ujerumani kwa kuchochea mapigano nchini Libya na kutojali vikwazo na marufuku ya kutopeleka silaha katika nchi hiyo iliyoathiriwa vibaya na vita.

Televisheni ya DW ya Ujerumani imeripoti kwamba, licha ya kuweko madai ya Ujerumaini ya kuheshimu vikwazo na marufuku ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kutopelekwa silaha huko Libya, lakini silaha nyingi zinazotumiwa nchini humo zinatokea Ujerumani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Uchumi ya Ujerumani, tangu kilipoitishwa kikao cha viongozi wa Libya miezi minne iliyopita, serikali ya Ujerumani imeshapeleka silaha zenye thamani ya dola milioni 331 huko Libya na kuzipa pande hasimu zinazoungwa mkono na nchi zenye uadui mkubwa baina yao za Misri, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Silaha za Wamagharibi ikiwemo Ujerumani zimeangamiza na kufanya uharibifu mkubwa nchini Libya

 

Ikumbukwe kuwa Uturuki inaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Sarraj ambayo inatambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, wakati mahasimu wakubwa wa Uturuki yaani Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri pamoja na Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Magharibi, zinamuunga mkono jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya."

Hivi karibuni kabisa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alizishutumu nchi zinazoyauzia silaha makundi hasimu nchini Libya na kuwaambia waandishi wa habari kuwa, kinachotokea Libya kinavunja moyo sana kwani madola mbalimbali hayaheshimu marufuku iliyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.