Kimbunga kikali chaua makumi ya watu India na Bangladesh
Kwa akali watu 20 wameaga dunia na mamia ya maelfu ya wengine wameachwa bila ya makazi baada ya kimbunga kikali cha Amphan kupiga maeneo ya pwani ya India na Bangladesh.
Kimbunga hicho kilichokuwa na upepo unaovuma kwa kasi ya kilomita 170 kwa saa kimeng'oa miti, milingoti ya umeme, mapaa na kuta za nyumba, huku kikisababisha kuripuka kwa mitambo ya kusambaza umeme katika pwani ya Bangladesh na mashariki mwa India.
Mamia ya nyumba ambazo nyingi kati yake ni za matope na vibanda zimebomolewa kutokana na kimbunga hicho kilichoambatana na upepo mkal katika pwani ya Bengal.
Waziri Kiongozi wa jimbo la Bengal Magharibi, mashariki mwa India amesema eneo hilo ndilo lililoathirika zaidi na tufani hiyo kwani watu wasiopungua 12 wameaga dunia, huku mifumo ya mawasiliano ikiharibiwa kikamilifu.
Maeneo hayo ya India na Bangladesh yamekuwa yakikumbwa na vimbunga mara kwa mara.
Novemba mwaka uliopita wa 2019, makumi ya watu walipoteza maisha na wengine zaidi ya milioni mbili waliachwa bila ya makazi kufuatia kimbunga kikali cha Bulbul kuyaathiri maeneo ya pwani ya India na Bangladesh huku kikiambatana na upepo mkali na mvua kubwa.
Watu zaidi ya 3,500 walifariki dunia kufuatia kimbunga kikali cha Sidr kilichopiga Bangladesh mwaka 2007.