Trump akosolewa na "Twitter" kwa kupotosha juu ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61239-trump_akosolewa_na_twitter_kwa_kupotosha_juu_ya_uchaguzi
Shirika la Twitter limemkosoa Rais Donald Trump wa Marekani kwa kuchapisha katika mtandao huo wa kijamii taarifa za kupotosha kuhusu uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 27, 2020 03:27 UTC
  • Trump akosolewa na

Shirika la Twitter limemkosoa Rais Donald Trump wa Marekani kwa kuchapisha katika mtandao huo wa kijamii taarifa za kupotosha kuhusu uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo.

Twitter imesema ujumbe wa Trump kwamba kufanyika uchaguzi wa Novemba mwaka huu kwa njia ya kutuma baruapepe kutasababisha uchakachuaji wa matokeo; hauna ukweli wowote. Trump anadai kuwa hizo ni njama za chama cha Democrats za kuiba kura katika uchaguzi huo.

Mwanasiasa huyo wa Repulican ameutishia na kuukosoa mtandao huo wa kijamii kwa kuuainisha ujumbe wake huo kuwa wa upotoshaji, na kuandika: Twitter inabinya kabisa uhuru wa kujieleza, na mimi kama Rais, sitokubali hilo lifanyike. 

Licha ya kuishambulia vikali Twitter, lakini rais huyo wa Marekani ni mraibu wa Twitter na amekuwa akiutumia mtandao huo wa kijamii kama jukwaa lake kuu la kutoa taarifa rasmi na zisizo rasmi, na hata kuwakebehi na kuwakejeli wapinzani na wakosoaji wake.

 

Trump mraibu mkubwa wa Twitter

Mapema mwaka huu, Trump aliweka rekodi katika urais wake ya kupitisha muda mwingi katika mtandao wa kijamii anaopendelea kuutumia wa Twitter baada ya kuandika na kutuma jumbe 125 sambamba na kuanza rasmi kesi ya kutaka kumuuzulu katika Seneti ya nchi hiyo.

Itakumbukwa kuwa, Disemba mwaka 2018, Trump aliishambulia vikali mitandao kadhaa ya kijamii kwa kuandika: "Facebook, Twitter na Google zinawapendelea Wademokrat, ni masikhara! Twitter imetia ugumu kwa watu kufuata ukurasa wangu na pia wamefuta akaunti nyingi."