Maandamano yaendelea Marekani, watu 13 wauawa, wanajeshi wajazwa mitaani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61389-maandamano_yaendelea_marekani_watu_13_wauawa_wanajeshi_wajazwa_mitaani
Wananchi wenye hasira Marekani wameendeleza maandamano kwa usiku wa sita mfululizo kulaani mauaji ya Mmarekani mweusi aliyeuawa kinyama mikononi mwa polisi mzungu wiki iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 03, 2020 05:41 UTC
  • Maandamano yaendelea Marekani, watu 13 wauawa, wanajeshi wajazwa mitaani

Wananchi wenye hasira Marekani wameendeleza maandamano kwa usiku wa sita mfululizo kulaani mauaji ya Mmarekani mweusi aliyeuawa kinyama mikononi mwa polisi mzungu wiki iliyopita.

Waandamanaji wamepambana na polisi katika miji mbali mbali nchini Marekani ambapo maandamano makubwa zaidi yameripotiwa Los Angeles, Philadelphia, Atlanta, Seattle na mji mkuu, Washington D.C. Kwa mujibu wa taarifa wanajeshi zaidi ya 1,600 wamepelekwa katika barabara za Washington D.C kukabiliana na waandamanaji. Aidha idadi kubwa ya wanajeshi na askari wa Gadi ya Taifa wametumwa katika miji mbali mbali kukabiliana na waandamanaji. 
Jumatatu ya wiki iliyopita, afisa mmoja mzungu wa jeshi la polisi la Marekani, anayejulikana kwa jina la Derek Chauvin, alimuua kikatili na kwa damu baridi kabisa, George Floyd Mmarekani mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis huku wenzake watatu wakitizama na kuwazuia wapita njia wasimuokoe Mmarekani huyo. Ukatili huo umezusha wimbi kubwa la maandamano na machafuko katika kona zote za Marekani na sasa Rais Donald Trump ametangaza serikali ya kijeshi.

Namna George Floyd alivyouawa kinyama na polisi mzungu nchini Marekani

Machafuko hayo yamechochewa zaidi na matamshi ya kijuba, kibaguzi na ya jeuri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump ambaye amewaita wanaolalamikia ukatili huo kuwa ni vibaka, wahuni na majambazi. Aidha hadi sasa watu 13 wameuawa kote Marekani katika maandamano ya kulaani mauaji ya Floyd huku hali ikiendelea kuwa mbaya. Utawala wa Marekani umelaaniwa kote duniani kwa kutumia mabavu kuwakandamiza waandamanaji wanaotetea haki.