Kashfa ya wapiga kura waliofariki katika uchaguzi wa rais Marekani
Kumepatikana idadi kubwa ya kura za watu waliofariki katika uchaguzi wa rais uliofanyika Jumanne nchini Marekani huku kukienea hofu ya kuwepo wizi wa kura katika uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya CNN ,wasimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Florida wanasema wametibua njama ya kutumiwa majina ya watu 50 kupiga kura katika jimbo hilo.
Aidha katika jimbo la New York gazeti la New York Post limeripoti kuwa kumepatikana kura ambazo zimetumwa kwa posa lakini majina ya waliopiga kura wameshafariki dunia.
Baada ya kampeni zilizokuwa na utata na vurugu, raia wa Marekani jana walipiga kura kumchagua rais mpya kati ya Donald Trump wa Republican anayewania muhula wa pili na mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden.
Ingawa jana ndiyo siku rasmi ya uchaguzi, watu wapatao milioni 100 tayari walikuwa wameshapiga kura ya mapema wakiwemo hao waliotumia njia ya posta kupiga kura.
Pamoja na kuwa raia wa Marekani wamejitokeza kupiga kura lakini kura zao haziamui mshindi katika uchaguzi.
Kwa mujibu wa sheria za Marekani, ili kuchaguliwa kuwa rais, mgombea anapaswa kupigiwa kura na jopo maalumu linalojulikana kama Electoral College lenye wajumbe 538.
Mshindi wa urais inabidi apate kura takribani 270 kutoka kwa wajumbe hao 538 kutoka majimbo mbali mbali ili kushinda uchaguzi.
Katika uchaguzi wa mwaka 2016, mpinzani Hillary Clinton, alipata kura nyingi za kawaida, ambapo alimzidi Trump kwa zaidi ya kura milioni mbili unusu kote nchini humo lakini Trump alinyakua urais kutokana na idadi kubwa ya kura katika jopo hilo. Wamarekani wengi wanakosoa mfumo huo wakisema si wa kidemokrasia na unawanyima haki ya kuwa waamuzi wa mwisho katika uchaguzi.