Biden kutazama upya uhusiano wa karibu wa Marekani na Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64642-biden_kutazama_upya_uhusiano_wa_karibu_wa_marekani_na_saudia
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa, Rais mteule wa nchi hiyo, Joe Biden anatazamiwa kuangalia upya uhusiano wa karibu uliopo hivi sasa baina ya nchi hiyo na Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 15, 2020 08:57 UTC
  • Biden kutazama upya uhusiano wa karibu wa Marekani na Saudia

Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa, Rais mteule wa nchi hiyo, Joe Biden anatazamiwa kuangalia upya uhusiano wa karibu uliopo hivi sasa baina ya nchi hiyo na Saudi Arabia.

Wataalamu na wadadisi wa mambo wamenukuliwa na mashirika ya habari ya Marekani wakisema kuwa, baada ya Biden kukabidhiwa hatamu za uongozi, Riyadh na Washington hazitakuwa tena na uhusiano wa kirafiki kama ilivyoshuhudiwa katika kipindi cha uongozi wa Donald Trump.

Shirika la NBC News la Marekani limefichua kuwa, Saudia haitastafidi tena na uhusiano mzuri na wa kidugu na Marekani kama ilivyoshuhudiwa katika kipindi cha Biden.

Biden amepania kuhitimisha vita vya muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen, ambavyo vimeua watu zaidi ya 112,000 tokea mwaka 2015. Kadhalika amedokeza kuwa utawala wake utasimamisha mauzo ya silaha kwa watawala wa Saudia.

Trump na Bin Salman

Mwanasiasa huyo wa chama cha Democratic amekuwa akiukosoa utawala wa kidikteta wa Riyadh kwa mienendo yake ya kukanyaga haki za binadamu, na hususan baada ya mauaji ya Jamal Khashoggi, aliyekuwa mwandishi wa habari na mkosoaji mkubwa wa wa ukoo wa Aal-Saud.

Trump alimkingia kifua wazi wazi Muhammad Bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudia, ambaye anatuhumiwa kutoa amri ya kutekelezwa mauaji hayo ya kikatili ya Oktoba mwaka 2018 katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki.